📌 Aatoa maagizo matatu kwa Wizara ya Maliasili

📌 Rais Samia aiweka Tanzania kwenye ramani ya utalii duniani

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa maonesho ya utalii ya Karibu– Kilifair yanaendelea kukuwa kimataifa na kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili fursa za biashara, kubadilishana uzoefu katika biashara za utalii na masoko pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hiyo muhimu ya uchumi.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Juni 6, 2025 jijini Arusha wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maonesho hayo ya kimataifa ya utalii ya Karibu -Kilifair 2025 yanayofanyika kuanzia Juni 5 hadi 7, 2025, yenye kaulimbiu “Utalii Endelevu, Kujenga Ustahimilivu na Ubunifu”.

“Kwa mwaka huu pekee, maonesho haya yamekutanisha waoneshaji zaidi ya 500 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na zaidi ya nchi 10 duniani, wanunuzi wa kimataifa 1,000 kutoka zaidi ya mataifa 40 pamoja na maelfu ya wadau na wataalamu wa sekta ya utalii. Hii ni dhahiri kuwa, dunia inaiangalia Tanzania na Afrika Mashariki kuwa kitovu cha utalii. Tutumie fursa hii kutangaza vitu tulivyonavyo,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema sekta ya utalii imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa maliasili na malikale, ustawi wa jamii na ukuaji wa kiuchumi. Ambapo takwimu zinaonesha kuwa, sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya mauzo ya nje.

Ameongeza kuwa Serikali inatekeleza programu mbalimbali za kimkakati za utangazaji utalii, zikiwemo filamu za Tanzania – the Royal Tour na Amazing Tanzania, ambazo zimeleta mafanikio makubwa kwa nchi.

Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko amesema Tanzania imeendelea kutambulika na kushinda tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo maarufu duniani za World Travel Awards – WTA zinazotolewa na Taasisi ya World Luxury Media Group Limited ya nchini Uingereza ambazo pia ni chachu katika kuvutia watalii katika soko la kimataifa.

“Tuzo hii ni matokeo ya Tanzania ya kutangaza ubora wa vivutio vilivyopo nchini kama vile Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro kuwa mahali bora pa kutembelea barani Afrika kwa shughuli za utalii wa safari na maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar. Pia, Tanzania imepewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za World Travel Awards kwa Kanda ya Afrika zitakazotolewa mwezi huu Juni, 2025,” amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kubuni njia mbalimbali za uendelezaji wa mazao ya utalii nchini kwa kuzingatia mgawanyiko wa aina ya mazao na mtawanyiko wa kijiografia wa nchi.

Maagizo mengine ni kutumia fursa za ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika utangazaji utalii na upatikanaji wa masoko ya utalii badala ya kutangaza kwa kutumia majarida pekee na kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara za utalii nchini ili kuchochea na kuvutia uwekezaji zaidi.

Halikadhalika ametoa rai kwa sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika sekta ya utalii hasa katika eneo la huduma za malazi, ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya soko kwa kuzingatia uwepo wa matukio mbalimbali ya kimataifa yanayoendelea kufanyika nchini.

Aidha, amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika nyanja mbalimbali ili kuhakikisha ustawi wa biashara za utalii nchini na maendeleo ya sekta kwa ujumla wake unanufaisha nchi. Sambamba na kuwataka Watanzania kuendelea kuwa wakarimu na kuelezea taswira nzuri ya nchi ili kuvutia wageni.

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wenye maoni na kukuza sekta ya utalii nchini.

Akielezea mafanikio ya sekta hiyo amesema inakuwa kwa kasi duniani hasa katika nchi mbalimbali mfano Tanzania ambapo mwaka 2024 imeingiza mapato ya utalii dola za marekani bilioni 3.9 pamoja na kupata watalii 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje 2,218,352.

Katika kuendelea kuimarisha sekta hiyo nchini, amesema Serikali imeridhia kujenga ukumbi mkubwa wa kimataifa jijini Arusha kwa gharama ya shilingi bilioni 230. Aidha, Wizara yake imeendelea kushirikiana na wadau ili kukuza biashara kwa kuwa na vikao na wadau hao ambapo imefanya maboresho ya sheria ya ada na tozo kwa lengo la kukuza sekta hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amewapongeza waandaji wa maonesho hayo ya Karibu – Kilifair na kusema kuwa ni kichocheo kikubwa cha uchumi mkoani humo, aidha amewaomba waandaji kuongeza idadi ya siku za maonesho kufikia siku tano hadi saba.

Balozi wa Shirikisho la Ujerumani nchini, Mhe. Thomas Terstegen amesema sekta ya utalii imesaidia kutoa ajira na kuongeza mapato nchini Tanzania. Aidha, nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali za utalii katika nchi za Afrika Mashariki ambapo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki wamezindua kampeni inayoitwa Visit East Africa Feel the Vibe ianyolenga kusaidia watalii kutembelea nchi za Afrika Mashariki.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Andrea Murietha amesema kuwa Jumuiya hiyo imeendelea kufanya jitihada za kutangaza utalii kwa kufanya kazi karibu na nchi wanachama ili kuhakikisha manufaa ya utalii yanapatikama kwa usawa katika nchi hizo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), Bw. Henry Kimambo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

“ Tunapokuwa na jambo kuhusu utalii tunasikilizwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi Taifa tunaishukuru sana Serikali kwa hili. Pia niiombe Serikali na wadau kwa pamoja tuongeze nguvu katika maonesho haya ili siku moja tushindane na yale ya Afrika Kusini, tunaweza kufanya haya maonesho ya Karibu- Kilifair kuwa makubwa zaidi Afrika,” amesema Kimambo.

Awali, Dkt. Biteko ametembelea mabanda mbalimbali ikiwemo banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ambalo kupitia banda hilo wametangaza fursa mbalimbali za uhifadhi na utalii kwa ajili ya kuvutia watalii na wawekezaji.

Vilevile, ametembelea banda la nishati (Energy solutions) ambapo wameonesha vifaa mbalimbali vinavyotumia nishati ya jua pamoja na banda la Hal linanalotengeneza magari yanayotumia umeme.