Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP kupitia mkandarasi wake Besix Ballast Nedam (BBN) imetoa ufadhili wa mafunzo stadi kwa wakazi 12 wa Kata ya Chongoleani panapojengwa miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta ghafi, hii ikiwa ni sehemu ya kuwajengea wananchi hao uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa ili kuwainua kiuchumi.

Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya ‘Local Content’ inayolenga kuwawezesha Watanzania kunufaiika na miradi mikubwa ya maendeleo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo iliyofanyika chuoni hapo jijini Tanga, Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii wa EACOP, Bi. Martha Makoi, alisema kuwa mradi huo si tu unahusika na ujenzi wa bomba la mafuta, bali pia unalenga kuacha alama ya maendeleo kwa Watanzania kupitia uwezeshaji wa rasilimali watu na uboreshaji wa huduma za kijamii.

Miongoni mwa wanufaika wa ufadhili wa mafunzo ya ufundi stadi yanayofadhiliwana mkandarasi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) Besix Ballast Nedam (BBN) Bi Fatuma Mohamed Salim akifafanua namna mafunzo hayo yatakavyobadilisha maisha yake wakati wa hafla fupi ya uzinguzi iliyofanyika katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Tanga, kulia ni Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii kutoka EACOP, Bi. Martha Makoi.

“Mradi huu ni wa kimkakati na unalenga kuwajengea uwezo Watanzania kupitia mafunzo, ajira na uboreshaji wa huduma,”

“Hadi sasa zaidi ya wanafunzi 200 wamefaidika na mpango huu kupitia mafunzo ya VETA na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadhi yao wamepewa ufadhili wa kusoma nje ya nchi,” alisema Bi. Makoi.

Naye Meneja wa Rasilimali Watu wa BBN, Bw. Harry Mangowi, alisema kuwa wakazi hao 12 wamefadhiliwa kusomea fani za Useremala, Ushonaji, pamoja na Ususi na Urembo, ili waweze kujiajiri na kuisaidia jamii yao.

“Mbali na kutoa ajira, tumeona ni vyema kuwajengea uwezo kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujitegemea,” amesema Bw. Mangowi.

Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), Bi. Martha Makoi (kushoto) akizungumza na wanufaika wa ufadhili wa mafunzo ya ufundi stadi ( hawapo pichani) yatakayotolewa kwa wakazi 12 wa Kata ya Chongoleani, katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Tanga, yaliyofadhiliwa na mkandarasi wake Besix Ballast Nedam (BBN) punde mara baada ya kuzinduliwa, jana. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho Bw. Gideon Lairumbe, wapili kulia ni ni Hubeir Rossano, Meneja EACOP.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Chuo hicho Bw. Gideon Lairumbe, alisema kuwa ushirikiano kati ya VETA na EACOP umekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu mafunzo hayo.

“Tunashukuru EACOP na BBN kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika mafunzo haya. Wanafunzi wanapopata mafunzo ya nadharia na vitendo, wanakuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa na taasisi mbalimbali, hivyo kusaidia ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alisema Bw. Lairumbe.

Mbali na ufadhili wa vijana, mkuu huyo pia ameishukuru EACOP kwa kutoa mafunzo kwa walimu wa chuo hicho na kuwezesha rasilimali vifaa vya kufundishia.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Chongoleani, Bw. Mohamed Salim, aliishukuru EACOP na mkandarasi BBN kwa kuendelea kutoa fursa za mafunzo na ajira kwa wananchi wa kata hiyo yenye vijiji vinne.

Viongozi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) na Mkandarasi wake Besix Ballast Nedam (BBN) wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi na uongozi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Tanga, punde mara baada ya hafla fupi ya uzinduzi wa ufadhili wa mafunzo kwa wakazi 12 wa kata ya Chongoleani kumalizika jijini humo.

“Tunashuhudia jinsi mradi huu unavyonufaisha jamii yetu. Mbali na kunufaika na ajira zisizohitaji ujuzi, vijana wetu pia wanapewa nafasi ya kupata mafunzo ya ufundi ambayo yanawawezesha kujitegemea,” alisema.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Bi. Fatma Salim kutoka Kijiji cha Ndaoya, alisema kuwa kabla ya kupata ufadhili alikuwa hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, lakini sasa ana matumaini makubwa ya kujiajiri kupitia fani ya ususi na urembo.

Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Peninsula ya Chongoleani, mkoani Tanga, na unapita katika mikoa minane nchini Tanzania ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Mradi huo unahusisha jumla ya wilaya 24, kata 134 na zaidi ya vijiji 180.

Wanahisa wa mradi huo ni TotalEnergies (62%), Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta Uganda (UNOC) kila moja ikiwa na asilimia 15, na Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya China (CNOOC) yenye asilimia 8.

Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), Bi. Martha Makoi (kushoto) akizungumza wakati wa kutembelea karakana Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Tanga inayotoa mafunzo kwa wakazi 12 wanaotoka kata ya Chongoleani panapojengwa gati ya kuhifadhia mafuta wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ufadhili wa mafunzo hayo, yaliyofadhiliwa na mkandarasi Besix Ballast Nedam (BBN) jana, kushoto ni Meneja wa Rasilimali Watu wa BBN, Bw. Harry Mangowi, wapili kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho Bw. Gideon Lairumbe na katikati Jerome Betht, Meneja wa kituo cha kuhifadhia mafuta cha Chongoleani (MTT).