Mataifa ya Afrika Magharibi yameamua kuunda kikosi cha wanajeshi 2,000 kukabiliana na makundi ya itikadi kali yanayozidi kuwa kitisho katika eneo hilo.
Afisa mmoja mkuu wa jeshi wa Nigeria aliliambia shirika la habari la AFP kwamba maamuzi kuhusu kikosi hicho kipya yalifanywa kwenye mkutano wa wakuu wa kijeshi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) nchini Sierra Leone uliomalizika Machi Mosi.
Afisa huyo alisema nchi kadhaa zilizoshiriki zilitangaza idadi ya wanajeshi zitakazochangia kikosi cha wanajeshi hao 2,000 ambao “watakuwa tayari kukabiliana na ugaidi na ukosefu wa usalama kote Afrika Magharibi.”
Chanzo chengine cha karibu na mazungumzo hayo kilisema wakuu wa majeshi walielezea hali ya wasiwasi ya usalama katika eneo hilo.
Hata hivyo, ECOWAS bado haijatoa tamko rasmi.



