Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TAASISI ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) imetoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzisha Kitengo Maalum cha Kitaifa cha Uchunguzi wa Watu Wanaopotea, kufuatia kuongezeka kwa matukio ya watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Hamis Msaoud amesema malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu watu kupotea yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, huku jamii ikianza kujenga imani kuwa hakuna jitihada za kutosha za kushughulikia matukio hayo.

Amesema kuwa licha ya Jeshi la Polisi kupitia makamanda wa mikoa kuthibitisha kupokea taarifa hizo na kudai kuwa uchunguzi unaendelea, bado kuna haja ya kuwa na chombo mahsusi chenye wataalamu waliobobea kushughulikia suala hilo kwa kina.

“Kutokana na mazingira yanayoendelea, ELAF tunaona umuhimu wa kuwa na kitengo maalum kitakachojikita kwenye uchunguzi wa watu wanaopotea,” amesema.

Ameongeza kuwa, wachunguzi wa kitengo hicho wanapaswa kuwa watu wenye vigezo madhubuti vya kitaaluma, afya bora, uwezo wa kiakili na uadilifu wa hali ya juu.

“Wachunguzi hao hawapaswi kuwa wa kufuata maelekezo ya mtu au kikundi chochote bali wafanye kazi kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, wakilinda utu wa kila mtu,” amesema.

Mkurugenzi huyo, amezitaja nchi kama Kenya, Mexico na Afrika Kusini kuwa tayari zimeanzisha vitengo maalum vya kushughulikia matukio ya watu wanaopotea, na hivyo Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwao katika kuimarisha mifumo ya haki na usalama kwa raia wake.

Aidha, amependekeza kuwa kitengo hicho kijumuishe wataalamu kutoka nyanja mbalimbali kama vile sheria, tiba ya afya ya akili, teknolojia ya habari na upelelezi wa kisayansi ili kuhakikisha matukio yanachunguzwa kwa weledi na ufanisi.

“Taasisi yetu itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na vyombo vya dola katika kuhakikisha kuwa suala la watu kupotea linapewa uzito unaostahili ili kulinda usalama na haki za binadamu nchini,” amesema.