Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
TAASISI ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) imetoa onyo kwa jamii kuhusu kuongezeka kwa kauli za udini ambazo zimeanza kujitokeza mara baada ya Uchaguzi Mkuu, ikisema mwelekeo huo unaweza kuleta athari kubwa kwa Taifa endapo hautadhibitiwa mapema.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 23, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dkt. Khamis Masoud, amesema Tanzania iko katika kipindi kinachohitaji maridhiano, ustahimilivu na mazungumzo, na si mazingira ya kugawana kwa misingi ya dini.
Ameongeza kuwa, kauli za udini si tu zinakosa hekima, bali zinaunda hofu, kuchochea chuki na kushusha imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
“Historia ya mataifa mbalimbali inaonyesha kuwa mfarakano wa kidini huanzia kwenye maneno madogo yanayopuuzwa na baadaye kugeuka misukosuko mikubwa inayodumu kwa miaka mingi.
“Kauli za udini haziwezi kutujenga. Ni maridhiano, haki na uadilifu ndivyo vitakavyoujenga upya moyo wa Tanzania. Taifa lisipojifunza kutoka historia yake, litajenga majeraha mapya… Maridhiano si udhaifu ni ujasiri wa kutengeneza kesho yenye umoja wa matumaini,” amesema.
Dkt Masoud ametumia rejea mbalimbali za kifalsafa kuonyesha kwamba udini hauendani na ustawi wa jamii ambapo amesema Falsafa ya Ubuntu inaeleza kuwa mwanadamu ni ndugu na si adui, jambo ambalo udini hulivunja.
“Aristotle anaamini taifa lenye afya linahitaji tabia njema, huku Rousseau akisisitiza kwamba serikali yenye uhalali ni ile inayounganisha wananchi wake,” amesema.
Aidha, Dkt. Masoud alirejea mawazo ya Kant kuhusu utu wa binadamu, akisema kauli zinazoigawa jamii kwa misingi ya imani zinadhalilisha msingi huo huku akikumbusha pia misingi ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyesisitiza kuwa Tanzania ilijengwa juu ya utu, usawa na mshikamano bila mipaka ya dini.
Katika hatua nyingine ELAF imeitaka serikali kuwa makini na matumizi ya lugha katika maeneo ya uongozi na mawasiliano kwa sababu maneno ya viongozi huwa dira ya taifa.
Pia, amewasihi viongozi wa dini kuhubiri umoja na upendo badala ya kutoa nafasi kwa misemo inayojenga hofu.
Kuhusu Vyama vya siasa amevitaka kuacha mara moja kutumia udini kama mtaji wa kisiasa, huku vijana wakihimizwa kutokubali kutumiwa kama chombo cha kugawa taifa.
Pia ameviomba Vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti lugha ya chuki na kusimamia maadili ya kiuandishi yanayolinda amani.
Vilevile, ELAF imependekeza kuanzishwa kwa majukwaa ya kitaifa ya mazungumzo, kuundwa kwa Tume ya Maridhiano, na kuimarisha elimu ya uraia inayoangazia amani na uzalendo.



