Na Fauzia Mussa, JamhuriMedia, Zanzibar
KAMISHENI ya kukabiliana maafa Zanzibar imehimizwa kuwa na Mipango madhubuti ya kupambana na majanga yatokanayo na kuzama majini kwa kutoa elimu kwa jamii, kuimarisha mifumo ya uokozi, na kuhimiza usalama wa maji.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh, wakati akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kuzuia kuzama majini duniani, yaliyofanyika katika fukwe za Forodhani, Unguja, yakibeba kaulimbiu yenye ujumbe “Hadithi Yako Inaweza Kuokoa Maisha.”
“Jamii yetu bado haina uelewa wa kutosha wa masuala ya usalama majini, wengi hawajui kuogelea na hata wanaojua hawawezi kujiokoa au kuwaokoa wengine kwa sababu hawana elimu ya uokozi,” alieleza.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kuendelea kushirikiana na vikosi vya uokozi kama KMKM na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU) kutoa elimu ya mara kwa mara kwa jamii, hasusan watoto, vijana, na wanawake ambao hushiriki shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii majini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya makamu wa Pili, Dk. Islam Seif Salum, alisema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kama vile kuandaa Sera ya Maafa ya mwaka 2025, ambayo ipo katika hatua za mwisho, ili kuzuia vifo vinavyotokana na kuzama majini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Makame Khatib Makame, alibainisha kuwa matukio ya watu kuzama yameendelea kujitokeza, hasa kwa watoto wa umri wa mwaka mmoja hadi 18, huku akitaja takwimu za Januari 2024 hadi Juni 2025 zilizoonesha matukio 29 yaliyohusisha watu 101 ambapo 78 walinusurika, wawili hawakuonekana, na 21 walifariki dunia.
Katika kuongeza uelewa, kamisheni hiyo imeshirikiana na wadau mbalimbali kuwafikia wakulima wa mwani, wanafunzi, waandishi wa habari na jamii za visiwa vya Uzi, Kizimkazi, Uvinje na Kisiwa Panza kwa elimu ya kujikinga dhidi ya kuzama.
Aidha, kamisheni ilitoa mapendekezo ya kuweka kingo kwenye mabwawa, walinzi kwenye fukwe za hoteli, na kujumuisha elimu ya uokozi na kuogelea kwenye mitaala ya shule za msingi na sekondari hasa ikizingatiwa Zanzibar imezungukwa na maji.

Mapema alieleza kuwa maadhimisho ya siku ya kuzuia kuzama yanalenga kuileta pamoja dunia Kwa kuandaa makongamano ya kuimarisha uelewa wa jamii juu ya changamoto za kiafya zinazoambatana na kuzama na kuweka njia madhubuti za kuzuia vifo vinavyotokana na kuzama na baadhi ya wakati kusababisha ulemavu hasa kwa jamii ilio katika mazingira hatarishi zaidi na watumiaji wakuu wa mazingira ya bahari, Mito na maziwa.
Wadau kutoka mashirika ya kimataifa kama WHO na UNICEF walisisitiza umuhimu wa kushajihisha Jamii Katika kuchukua hatua za kujikinga na kuzama wakisisitiza kuwa vifo vinavyotokana na kuzama ni tatizo linalozuilika endapo elimu na hatua za kinga zitachukuliwa kwa pamoja.
Mwakilishi wa shirika la Afya ulimwenguni (WHO) Dk. Ali Omar alieleza dhamira ya who ya kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Katika kuijengea uwezo Jamii wa masuala ya usalama majini na kubainisha kuwa baadhi ya nchi zimefanikiwa kupunguza viwango vya vifo vitokonavyo na kuzama majini kupitia utekelezaji wa hatua za kinga.
Ofisa wa shirika linalohudumia watoto ulimwenguni UNICEF Upande wa zanzibar, Marco Msambazi alisema wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali Katika kuhakikisha wanaokoa maisha hasa ya watoto ambao wanachukulia michezo ya majini kama sehemu yao ya maisha.

Mkurugenzi wa Chuo cha Uokozi Zanzibar, Lukman Saidi Issa, alitaja sababu kuu zinazochangia hatari ya kuzama kuwa ni ukosefu wa uangalizi kwa watoto, kusafiri kwa boti zilizojaa kupita kiasi, uvuvi wa kienyeji wakati wa dhoruba, na uhamiaji haramu kupitia bahari.
Maadhimisho hayo yaliambatana na zoezi la kuzama na uokozi na mashindano ya kuogelea kwa makundi mbalimbali likiwemo la watu wenye ulemavu yakilenga kuhamasisha usalama majini kwa njia shirikishi na kuibua vipaji vya uokoaji wa maisha majini .


