Mataifa yenye nguvu barani Ulaya yameonya jana kuwa vitisho vya ushuru vya Rais wa Marekani Donald Trump juu ya Greenland vinahatarisha hali ya kiuchumi wakati yakijaribu kupima jibu la mzozo huo unaopanuka.

Katika taarifa ya pamoja, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Sweden na Uingereza zimesema vitisho hivyo vya kibiashara vinavyohusishwa na nia ya Trump kuchukua udhibiti wa Greenland pia vinadhoofisha mahusiano ya mataifa ya eneo la Atlantiki.

Zimesema zitadumisha umoja na uratibu katika jibu lao na kwamba pia zimejitolea kuzingatia uhuru wao.

Wakati huo huo, afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya amesema Rais wa Baraza la Umoja huo António Costa ataanda mkutano maalumu wa kilele kufuatia vitisho hivyo vya ushuru vya Trump.

Costa amesema mashauriano yake na nchi wanachama yameweka wazi kuwa ushuru huo hauendani na makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.