Wabunge wa Umoja wa Ulaya wameamua kuahirisha kupitishwa kwa mpango wa kibiashara kati ya umoja huo na Marekani kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu sera ya ushuru ya Rais Donald Trump.
Hii inajiri baada ya Trump kutangaza ushuru mpya wa jumla wa asilimia 15 kama jibu la uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Marekani wiki iliyopita ambao ulifuta ushuru wake wa awali aliotangaza duniani kote.
Kamati ya biashara ya Bunge la Ulaya ilipanga kupiga kura Jumanne ili kuondoa ushuru kwenye bidhaa za viwandani za Marekani. Lakini kura hiyo sasa imeahirishwa. Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Olof Gill alisema Brussels haiwezi kuchukua maamuzi zaidi hadi itakapopata ufafanuzi kutoka Washington.
Rais wa Halmshauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen alifikia makubaliano na Trump mwezi Julai mwaka jana kwa ajili ya ushuru wa juu wa asilimia 15 kwa bidhaa nyingi za Ulaya zinazokwenda Marekani. Brussels pia ilikubali kuondoa ushuru mwingi wa bidhaa zinazoingizwa Umoja wa Ulaya kutoka Marekani.
Mkataba huo ambao ni wa kisheria unahitaji kuidhinishwa na Bunge la Ulaya na serikali za Umoja wa Ulaya. Ushuru wa hivi karibuni wa asilimia 15 uliotangazwa na Trump unaanza kutekelezwa leo Jumanne. Unaweza kutekelezwa kwa siku 150 pekee isipokuwa tu kama Bunge litaongeza muda.


