Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, leo Agosti 5, 2025 ametembelea banda la Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, ambapo ametoa wito kwa Baraza hilo kuimarisha elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa wa huduma hizo muhimu.

Akiwa kwenye banda hilo, Senyamule amepokea maelezo kutoka kwa Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Lugiko L. Lugiko, kuhusu huduma zinazotolewa na Baraza hilo, ikiwemo kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mafuta, gesi, umeme na maji hatua inayotajwa kuwa ni chachu ya kuongeza ufanisi na uwazi katika sekta hizo nyeti .

Lugiko ameeleza kuwa ushiriki wa EWURA CCC katika Maonesho ya Wakulima mwaka huu ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi, hususan wale wa maeneo ya pembezoni, ambao mara nyingi hukosa taarifa sahihi na mwongozo wa namna bora ya kushughulikia changamoto na malalamiko yanayohusiana na huduma za nishati na maji.

Kutokana na hayo Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amepongeza ubunifu huo wa EWURA CCC na kueleza kuwa kutoa elimu ya moja kwa moja kwa wananchi ni njia bora ya kuwajengea uwezo wananchi wa kutambua haki na wajibu wao, hatua ambayo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kupitia matumizi sahihi na endelevu ya nishati na maji.

Senyamule amesisitiza umuhimu wa Baraza hilo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, ufuatiliaji wa bei za mafuta na huduma za maji na umeme, ili wananchi wa vijijini waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo na biashara kwa tija zaidi.

Aidha, ametoa ushauri wa EWURA CCC kuendelea kutumia fursa za maonesho kama haya kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa matumizi salama ya nishati, ufuatiliaji wa bei na udhibiti wa huduma za maji ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya kilimo na ustawi wa wananchi.

Katika kuongeza ufanisi wa huduma hizo, Senyamule amewaagiza wataalamu wa EWURA kutumia majukwaa Jukwaa la Nanenane
Maonesho ya Nanenane, yanayofanyika kila mwaka, yamekuwa kiunganishi muhimu kati ya serikali, wakulima na wadau wa maendeleo. Katika maonesho ya mwaka huu yenye kauli mbiu “Kilimo Bora, Uchumi Imara”, EWURA CCC imeendelea kutoa mafunzo ya moja kwa moja kwa wakulima kuhusu bei sahihi za mafuta, hatua za kushughulikia bili zisizoeleweka, na namna ya kushirikiana na wadhibiti ili kuhakikisha huduma bora.

Banda la EWURA CCC limekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa vikundi vya wanawake, vijana na wakulima wadogo, kuhusu huduma za nishati na maji zinavyoweza kuongeza thamani ya mazao kupitia kilimo cha kisasa na matumizi ya gesi asilia katika usindikaji wa mazao.

Wananchi waliotembelea banda hilo wamepongeza jitihada hizo, wakisema elimu hiyo itasaidia kupunguza changamoto walizokuwa wakizipata kwa miaka mingi.

Grace Ntembo, mkulima kutoka wilayani Busega amesema: “Kupitia EWURA CCC tunajua sasa namna sahihi ya kushughulikia changamoto za maji na umeme vijijini.”

EWURA CCC imeahidi kuendeleza mikakati ya kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu na ushawishi wa watumiaji wa huduma za nishati na maji unawafikia Watanzania wote, hatua inayotarajiwa kuchochea uwajibikaji na uboreshaji wa huduma kwa manufaa ya taifa.