Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Kaimu  Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, amesema taasisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  hiyo inafanya uchunguzi wa vifurushi vya mtandao (internet) ili kubaini kama wananchi wanarubuniwa katika gharama na matumizi ya vifurushi hivyo.

Ngasongwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari  kwamba kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu vifurushi vya bando kunalizika kwa muda mfupi licha ya gharama kubwa ya bando.

Aidha alisema FCC inaendelea kusimamia ushindani wa haki katika sekta mbalimbali za uchumi ili kulinda maslahi ya wananchi na kukuza uwekezaji nchini.

Taasisi hiyo  imeendelea kuridhia miungano na ununuzi wa makampuni mbalimbali baada ya kujiridhisha kuwa hatua hizo hazitakiuka misingi ya ushindani wa haki sokoni, huku zikichochea uwekezaji na maendeleo ya sekta tofauti.

Akizungumzia sekta ya mawasiliano, Ngasongwa alisema Tume ya Ushindani iliridhia ununuzi wa kampuni ya Habari Node Limited, inayojihusisha na utoaji wa huduma za intaneti kwa njia ya Fiber na Wireless katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Tanga na Mara.

Alisema kampuni hiyo imenunuliwa na Pembani Remgro Infrastructure Fund II, ambao ni mfuko wa uwekezaji wa kibinafsi unaojishughulisha na uwekezaji wa hisa katika makampuni mbalimbali barani Afrika.

Kwa mujibu wa Ngasongwa, muungano huo unatarajiwa kuiwezesha Habari Node Limited kupata mtaji utakaosaidia kuongeza ufanisi katika shughuli zake nchini pamoja na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za intaneti ya bei nafuu na inayotegemewa kwa wananchi.

Katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa viwandani, Ngasongwa alisema FCC iliridhia ununuzi wa makampuni saba yaliyoko katika sekta hiyo kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 103.9, ambapo makampuni hayo yamenunuliwa na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema makampuni hayo yanajihusisha na uzalishaji na uchakataji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni, vifaa vya usambazaji wa maji, vifungashio, bidhaa za karatasi, malighafi za plastiki, polima pamoja na rangi changanyiki za plastiki.

Ngasongwa alieleza kuwa miongoni mwa miungano iliyopata ridhaa ya FCC ni ununuzi wa kampuni ya PLASCO Limited inayozalisha vifaa vya usambazaji wa maji kama matangi ya kuhifadhia maji pamoja na mabomba ya HDPE na uPVC, ambapo kampuni hiyo ilinunuliwa na Super Commodity Solutions Co. Limited na Sun Energies Industries Limited.

Alisema muungano huo unalenga kuongeza upatikanaji wa rasilimali za kifedha, kiutendaji na kimkakati ili kuendeleza na kupanua shughuli za uzalishaji wa kampuni hiyo.

Aidha, kampuni ya kimataifa ya Guala Closures S.p.A inayobobea katika utengenezaji wa vifuniko na vizibo vya chupa ilinunua kampuni ya Metal Crowns (Tanzania) Limited (MTCL), inayojishughulisha na uzalishaji wa vifuniko vya chupa.

Ngasongwa alisema muungano huo unatarajiwa kuboresha ufanisi wa kiutendaji wa kampuni hiyo pamoja na kuimarisha uwezo wake wa kuhudumia wateja wanaotumia bidhaa za kufungia chupa.

Katika hatua nyingine, kampuni ya Sunrise Enterprises Limited ilinunua kampuni ya Fortune Paper Group Limited ambayo inamiliki kiwanda cha kuchakata karatasi chakavu kinachotumika kama malighafi kuu kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali za karatasi.

Alisema muungano huo unatarajiwa kuongeza mtaji pamoja na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho kutoka tani 12,000 hadi tani 60,000 kwa mwaka.

Ngasongwa alibainisha kuwa kwa ujumla kuridhiwa kwa miungano hiyo katika sekta ya uzalishaji viwandani kunalenga kuongeza mitaji ya makampuni, kupanua uzalishaji na usambazaji wa bidhaa, kuboresha ufanisi wa kiutendaji kwa kutumia teknolojia na utaalam mpya, pamoja na kuimarisha ushindani wa haki sokoni.

Alisema hatua hizo pia zinachangia kuongeza ajira, kukuza uchumi wa taifa na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na nafuu.

Kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia, Ngasongwa alisema FCC inaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963 ambayo inalenga kuzuia uingizaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa bandia au zenye maelezo potofu.

Alisema bidhaa bandia huzuia ushindani wa haki, kuathiri biashara halali na kuwahadaa watumiaji, hali inayoweza kuleta mazingira yasiyo sawa katika soko.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unasaidia kuhakikisha biashara zinashindana kwa misingi ya ubora, ubunifu na kufuata sheria badala ya udanganyifu, hatua inayochangia kujenga soko lenye uwazi na ushindani wa haki.

Ngasongwa alisema udhibiti wa bidhaa bandia pia unachangia kukuza uchumi kwa kuwa biashara halali hubaki na mapato yao, jambo linalochochea uwekezaji, kuongeza ajira na kuendeleza ubunifu.

Alisema jitihada hizo pia zinawalinda watumiaji dhidi ya bidhaa zisizo salama au zisizo halisi, huku zikiboresha sifa ya biashara za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.