Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Mradi mpya wa Misitu na Matumizi ya Ardhi na Maendeleo ya Myororo wa Thamani (FORLAND) umejizatiti kuhakikisha miradi ya misitu inakuwa na tija kwa wananchi kuanzia hatua ya upandaji hadi mlaji wa mwisho.
Mradi huu mpya, unaofadhiliwa kwa pamoja kati ya Seikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Finland, unatokana na mafanikio ya Mpango Shirikishi wa Upandaji Misitu (PFP2) na Mpango wa Kukuza Misitu na Mnyororo wa Thamani (FORVAC).
Kati ya matarajio ya mradi huu ni uboreshaji wa usimamizi wa misitu ya wakulima wadogo wadogo, kuongezea taasisi mbalimbali uwezo wa kielimu, kuimarisha uhusiano kati ya sekta binafsi na sekta ya uma ili kuboresha sera ya misitu kwenye mnyororo mzima wa misitu.

Akizungumza katika kilele cha maonesho ya Nane Nane mjini Dodoma, Mratibu wa Mradi wa Taifa wa FORLAND, Emma Nzunda alisema mradi huo umepokewa vizuri na wananchi kwa kuzingatia mafanikio yaliyopatikana katika miradi iliyopita.
“Tuko hapa Nane Nane kutambulisha FORLAND ili wananchi wengi zaidi waufahamu na uwasaidie mwananchi mmoja mmoja katika uhifadhi wa misitu na matumizi bora ya ardhi,” alisema.
Aliongeza kuwa mradi huu haulengi tu usimamizi bora wa misitu lakini pia unaimarisha minyororo ya thamani-kusaidia jamii, wawekezaji kwenye mashamba ya miti, na wafanyabiashara wadogo na wa kati katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu wanayozalisha”, alibainisha Nzunda.
Kwa mujibu wake, FORLAND inafungamana kwa karibu na vipaumbele vya maendeleo vya serikali ya Finland na Tanzania na inachangia katika kupunguza umaskini, kuzalisha ajira, na kuimarisha ustahimilivu wa hali ya hewa.
Miongoni mwa matokeo muhimu yanayotarajiwa kutokana na mradi huo ni pamoja na uboreshaji wa usimamizi wa mashamba ya miti ya wakulima wadogo wadogo, uimarishaji wa kitaasisi katika elimu ya misitu, na kuongezeka kwa mazungumzo kati ya wadau wa umma na binafsi ili kuboresha mazingira ya sera ya misitu.
“Mradi pia unalenga kuongeza uwezo wa wakulima wa miti na mashirika yao kusimamia mashamba kwa ufanisi zaidi na kupata mavuno bora,” Nzunda alisisitiza kuwa misitu ni uchumi na hela hasa ukisimamiwa vizuri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu (FWITC), Bertha Nyodewa alisema kituo hicho kinafanya kazi kwa karibu na FORLAND ili kuwapa wakulima maarifa na utaalamu zaidi.
“Tunahitaji kuongeza uelewa kuhusu miche bora, usimamizi endelevu wa misitu, mipango ya matumizi mazuri ya ardhi na jinsi upandaji miti unavyoweza kuwa biashara yenye faida,” alisema.

Mjumbe wa Chama cha Wakulima wa Miti Tanzania (TTGAU), Kastory Timbula, alieleza kufurahishwa kwake na mradi huo ambao umewaongezea wakulima wengi wa misitu maarifa kuhusiana na kilimo hicho.
Alisema hatua iliyochukuliwa na FORLAND ya kuweka uzito katika mnyororo wa thamani kwa kupitia vikundi vya akina mama na vijana itasaidia vikundi hivi kuanzisha shughuli nyingine zenye faida kama vile ufugaji wa nyuki, utengenezaji wa vikapu na uuzaji wa asali.