Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Kampuni ya Fortune Paper Group inayomilikiwa na wawekezaji wa China, imeiomba Serikali kuweka sera madhubuti zitakazolinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani unaotokana na bidhaa za bei nafuu zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Kampuni hiyo, ambayo imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 154 nchini Tanzania tangu mwaka 2022, imesema kuwa hali ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje bila udhibiti wa kutosha inaleta ushindani usio wa haki na kuhatarisha ukuaji wa viwanda vya ndani, hasa vile vinavyohusika na urejelezaji.
Akizungumza Machi 30, 2026 jijini Dar es Salaam, Meneja wa Biashara wa kiwanda hicho, Colin Yang, alisema Serikali ina wajibu wa kuangalia namna ya kusaidia sekta ya uzalishaji wa ndani kupitia sera zitakazoweka uwiano sawa wa ushindani sokoni.
Alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalum yaliyofanyika pembeni ya maonesho ya Siku ya Kimataifa ya Zero Waste (Taka ni Ajira) yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Yang alisema licha ya kampuni hiyo kulipa kodi stahiki, bado inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa bidhaa za karatasi zinazoagizwa kutoka nje, hasa kutoka India na China, ambazo huingia nchini kwa utaratibu wa msamaha wa ushuru, hivyo kuzikwepa gharama wanazobeba wazalishaji wa ndani.
Alieleza kuwa Fortune Paper hukusanya karatasi taka kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuzigeuza kuwa bidhaa za kufungashia kama maboksi, bahasha na bidhaa nyingine za viwandani.
“Hii ndiyo malighafi yetu; kwetu taka ni mali. Tunakusanya karatasi taka kote nchini na kuzibadilisha kuwa bidhaa mbalimbali za vifungashio,” alisema Yang.
Aliongeza kuwa uwekezaji huo sio tu unalenga faida ya kibiashara, bali pia unachangia katika uhifadhi wa mazingira kupitia ajenda ya urejelezaji nchini.
Kwa mujibu wa Yang, tangu kuanza shughuli zake mwaka 2022, kampuni hiyo imewekeza zaidi ya dola milioni 60 katika kuimarisha uzalishaji na shughuli zake za ndani, huku ikiajiri zaidi ya wafanyakazi 150 wazawa.
Alisema kampuni ina mipango ya kuongeza uzalishaji pamoja na kupanua uwekezaji wake, kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa za ndani katika siku zijazo.
Maonesho hayo yalikuwa sehemu ya kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Zero Waste, yaliyohudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Hamad Yusuf Masauni.



