Na Mwandishi wetu, JahuriMedia, Mirerani
KAMPUNI ya Franone Mining LTD, inajenga zahanati ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, hivyo wachimbaji kuondokana na changamoto ya huduma za afya..
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala akizungumza na wachimbaji baada ya kukagua ujenzi wa zahanati hiyo itakayogharimu Sh180 milioni inajengwa kupitia uwajibikaji kwa jamii (CSR), ameipongeza kampuni ya Franone.
DC Lulandala ameeleza kwamba zahanati hiyo itakayowanufaisha wachimbaji hao imejengwa na Franone mining kupitia uwajibikaji kwa jamii (CSR) na itakapokamilika itaanza kutoa huduma za afya kwa wadau wa madini.
Ameeleza kwamba zahanati hiyo itakamilika baada ya miezi mitatu, wadau wa madini ya Tanzanite wa eneo hilo watapatiwa huduma za afya kwa urahisi baada ya kupangiwa wataalamu wa afya.
“Nimeshamuagiza mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya (DMO) kuandaa mganga wa zahanati, nesi na mtaalam wa dawa ili zahanati ikikamilika ianze kazi mara moja,” amesema DC Lulandala.
Amesema changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya kwenye eneo hilo ni ya muda mrefu ila baada ya kukamilika kwake wachimbaji watapata huduma.
“Franone wametuwahi tuu kwani serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilikuwa na lengo la kujenga zahanati huku migodini,” amesema DC Lulandala.
Meneja mkuu wa kampuni ya Franone mining Vitus Ndakize amesema wanajenga zahanati hiyo kwa lengo la kuhudumia jamii kupitia CSR na ujenzi wake umefikia asilimia 26.
Ndakize amesema pamoja na kuwa wamesaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ya CSR ya eneo hilo wameona kwa wakati huu ni vyema wakajenga zahanati ili kusaidia wachimbaji kwa upande wa afya.
“Zahanati hii itakapokamilika pia kutakuwa na vyumba kwa ajili ya wataalam wa kifua kutoka hospitali ya kifua kikuu ya Kibong’oto watakaofanya kliniki ya magonjwa ya kifua,” amesema.
Mhandisi wa majengo wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Grace Munuo ameeleza kwamba huwa wanakagua ujenzi unavyoendelea na endapo kukilazimika kufanyika kwa marekebisho wanaelekeza na kufanyika.
Munuo amesema kwa namna ujenzi unavyofanyika wana uhakika jengo hilo la zahanati litakamilika kwa muda wa miezi mitatu kama ilivyopangwa.
Wadau wa madini ya Tanzanite wa kitalu D na kitalu B (Opec) wamepongeza hatua hiyo kwani hawana hospitai, kituo cha afya wala zahanati katika eneo hilo, hivyo wanawashukuru Franone kwa kujenga zahanati hiyo.

