Watanzania Watakiwa Kuzichangamkia
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Sekta ya madini nchini Tanzania inaendelea kushamiri kwa kasi, ikifungua milango ya ajira, uwekezaji na maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kuhakikisha usimamizi madhubuti, uwazi, na ushirikishwaji wa wadau wote katika mnyororo mzima wa shughuli za madini. Haya yamekuwa ni matokeo ya maboresho ya sera, sheria, pamoja na mifumo ya kidijitali inayotumika katika kusimamia sekta hiyo.

Akizungumza leo Juni 21, 2025 katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Afisa Ukaguzi Migodi kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Bw. Ashen Mwambage, amesema kuwa Watanzania wengi wanapaswa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa kupitia Sekta ya Madini.
Ameeleza kuwa katika mikoa mbalimbali kama Geita, Shinyanga, Mara na Mbeya, wananchi wamehamasika kushiriki katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato cha familia na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha fursa hizi zinamfikia kila Mtanzania. Kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali, sasa bei ya madini iko wazi, mapato ya Serikali yanaongezeka na wachimbaji wananufaika kwa haki,” amesema Bw. Mwambage.

Kwa upande wa teknolojia, amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele kusukuma matumizi ya mbinu za kisasa katika utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kuongeza ufanisi, kupunguza athari za mazingira na kuhakikisha usalama kwa wachimbaji wadogo. Hii imeenda sambamba na utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara kwa wachimbaji hao.
“Hatupaswi kuuza madini ghafi, bali kuongeza thamani hapa hapa nchini. Uongezaji thamani madini umefungua fursa nyingi za ajira, ujasiriamali, na kuinua Pato la Taifa,” ameongeza.

Aidha, Bw. Mwambage amesema kuwa mchango wa Sekta ya Madini umeendelea kuibua fursa kwenye sekta nyingine kama uchukuzi, huduma za malazi, usafirishaji wa mizigo, huduma za kifedha na bima, hali inayoonesha namna sekta hiyo inavyobeba uchumi wa nchi kwa mapana yake.
Tume ya Madini inatoa wito kwa Watanzania wote, hususan vijana, kuchangamkia fursa zilizopo kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa ili waweze kunufaika na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
