Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetoa wito kwa wananchi, wajasiriamali na wanafunzi kutembelea banda lao katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (DITF – Sabasaba) ili kujifunza kuhusu usalama wa kemikali, usajili, na mchango wa Sayansi katika kulinda afya ya jamii.

Akizungumza katika banda hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt. Peter Shimo, amesema GCLA inashughulika na uchunguzi wa sampuli mbalimbali kama zile zinazotokana na jinai, mazingira, tiba na DNA.

“Huduma tunazotoa ni pamoja na usajili wa kemikali, kutoa elimu kwa wananchi na kuwasaidia wajasiriamali wanaojihusisha na bidhaa za kemikali kutambua njia sahihi za usajili. Kwa wale walioko mbali, tunawashauri watumie tovuti yetu au kufika kwenye banda letu kwa msaada wa moja kwa moja,” alisema Dkt. Shimo.

Ameeleza pia kuwa mamlaka hiyo ni msaada mkubwa kwa jamii hasa katika kudhibiti kesi za kihalifu zinazohusiana na kemikali haramu kama bangi, ambapo sampuli huchunguzwa kitaalamu ili kuthibitisha ushahidi wa kisayansi.

Aidha, Dkt. Shimo amewakaribisha wanafunzi wanaopenda masomo ya Sayansi kutembelea banda hilo ili kujifunza kuhusu taaluma ya uchunguzi wa kisayansi.

“Kila mwaka huwa tunatoa zawadi kwa mwanafunzi anayeonyesha juhudi. Hii ni sehemu ya kuwahamasisha vijana wetu kuipenda Sayansi na kujua kuwa taaluma hii ina nafasi muhimu katika maisha ya kila siku,” alisisitiza.

Mamlaka hiyo imesema inatarajia kuona mwitikio mkubwa wa wananchi kutembelea Maabara baada ya maonesho haya, ili kuendeleza elimu na usalama wa jamii dhidi ya kemikali hatarishi.

Kwa upande wake, Hassan Zakimu, mkazi wa Dar es Salaam aliyeitembelea banda hilo, amesema amejionea kazi kubwa inayofanywa na GCLA.

“Kwa kweli wanasaidia sana jamii. Kazi yao inalinda afya zetu kwa kutambua kemikali hatarishi na kusaidia hata kwenye kesi za jinai,” alisema.