Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika miji mikuu nchini Kenya kukumbuka tukio la Juni 25 mwaka uliopita ambapo wenzao 60 waliuawa na Polisi wakati wa maandamano ya kuupinga Mswada wa Fedha mwaka 2024.

Hata hivyo Polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwakabili waandamanaji katika Jiji la Nairobi, huku usalama ukidumishwa katika majengo ya serikali.

Anga ya taharuki na moshi ya mabomu ya kutoa machozi ilitanda katika miji ya Nairobi, Mombasa, Nakuru na maeneo mengine ya Kenya huku waandamanaji wakijitokeza kwa wingi katika siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja baada ya vijana wa Gen-Z kuuawa kwenye tukio la kihistoria walipolivamia bunge la taifa la Kenya.

Waandamanaji hao waliokuwa wakielekea katika kituo kikuu cha Polisi cha Nairobi alikofia Albert Ojwang walikabiliwa na polisi wa kupambana na ghasia huku wakiwarushia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Barabara kuu za kuingia jijini zilifungwa na polisi kuwazuia waandamanaji kuingia Katikati mwa jiji. Maduka mengi yalifungwa kwa hofu ya uhalifu. Mtu mmoja amejeruhiwa kwenye vurugu hizo.