Accra, Ghana
NCHI za Ghana na Tanzania zinaendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi katika utekelezaji wa sera za Ushirikishwaji wa Wazawa katika Sekta ya Madini (Local Content), kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi wa ndani katika minyororo ya thamani ya madini, kuimarisha uwezo wa taasisi za ndani na kuhakikisha manufaa ya kiuchumi yanabaki ndani ya nchi.
Hayo yalibainishwa katika ziara rasmi ya kubadilishana uzoefu kati ya wawakilishi wa Tume ya Madini ya Tanzania na Tume ya Madini ya Ghana, iliyolenga kujifunza na kushirikishana mbinu bora, sera na mifumo ya utekelezaji wa Local Content katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia C. Numbi, amesema kuwa sera ya Local Content si takwa la kisheria pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya taifa, ujenzi wa viwanda na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wananchi.
“Ningependa kusisitiza kuwa Maudhui ya Ndani katika sekta ya madini ni msingi imara wa maendeleo ya taifa, viwanda na uwezeshaji wa kiuchumi nchini Tanzania. Sera ya Madini ya mwaka 2009, Sheria ya Madini Sura ya 123, pamoja na Kanuni za Mining (Local Content) za mwaka 2018, zinaitaka Tume ya Madini kuratibu, kusimamia na kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa Maudhui ya Ndani katika mnyororo mzima wa thamani ya madini,” amesema Dkt. Numbi.
Ameipongeza Tume ya Madini ya Ghana kwa ukarimu na mapokezi mazuri, huku akiainisha mafanikio yaliyopatikana nchini Tanzania ambapo ajira kwa Watanzania katika sekta ya madini zimefikia asilimia 98, huku ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani ukiongezeka hadi asilimia 88 kufikia mwaka 2025.
Dkt. Numbi amesema ziara hiyo itaweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu na wa kimkakati kati ya Tume ya Madini ya Tanzania na Tume ya Madini ya Ghana, ambao pia utakuwa rejea muhimu kwa nchi nyingine za Afrika katika utekelezaji wa sera za Local Content.
“Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kujenga sekta ya madini endelevu barani Afrika, itakayochangia ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya kijamii,” ameongeza.
Ameeleza kuwa makubaliano ya ushirikiano yatatekelezwa kupitia programu za mafunzo ya pamoja, kubadilishana wataalam, pamoja na kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kuhakikisha manufaa ya rasilimali madini yanawanufaisha kikamilifu wananchi wa ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Madini ya Ghana, Bw. Isaac Tandoh, ameukaribisha ujumbe kutoka Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya madini.
Amesema ushirikiano huo unalenga kubadilishana maarifa, teknolojia na uzoefu katika udhibiti, uchimbaji na biashara ya madini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kukuza maendeleo endelevu ya sekta ya madini barani Afrika.
Katika ziara hiyo, wataalam kutoka pande zote mbili wamejadili masuala muhimu ikiwemo ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu, uhamishaji wa teknolojia, mipango ya urithi wa maarifa, pamoja na mifumo bora ya ufuatiliaji na uwajibikaji, kwa lengo la kukabiliana na changamoto kama vile utafiti mdogo wa madini na maendeleo ya viwanda vya kuongeza thamani zaidi.


