Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

CHUO Kikuu cha Mzumbe cha mkoani Morogoro na Wakala wa Elimu Nje ya Nchi (Global Education Link), wamesaini Mkataba wa Ushirikiano (MoU) kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa fursa za elimu nje ya nchi.

Mkataba huo ulisainiwa jana katika ofisi za GEL jijini Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi Mkuu wa GEL Abdulmalik Mollel na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa William Mwegoha.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Mollel alisema lengo la makubaliano hayo ni kuongeza ufahamu kwa wanafunzi na wahadhiri wa chuo hicho kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kimataifa.

Alisema GEL imetengeneza mfumo kidijitali wanaoutumia kufuatilia na kupata taarifa mbalimbali za vyuo vikuu nje ya nchi pamoja na kufuatilia maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi wanaowapeleka nje ya nchi.

Alisema GEL imekuwa ikiwaambia wanafunzi wanaokwenda nje ya nchi mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya safari, wakati wa safari na hata baada ya kufika kwenye nchi wanazokwenda hasa kuzingatia masomo.

Mollel alisema wamekuwa wakiwasisitiza wanafunzi hao kuachana na biashara na mambo ya anasa ambayo yanaweza kuwapotezea malengo kwenye masomo.

“Kwa kutumia mfumo huu, tunahakikisha tunapata taarifa sahihi za vyuo na tarifa za maendeleo ya kila mwanafunzi tuliyempeleka nje ya nchi kwasababu taarifa zote zinaletwa kwa wakati, hivyo kuongeza uwazi na ufanisi katika huduma zetu,” alisema Mollel.

Alisema MoU hiyo itasaidia kupanua programu za kubadilishana wanafunzi na wahadhiri baina ya chuo hicho na vyuo vikuu vya nje ya nchi na kuwezesha tafiti za pamoja.

Alisema makubaliano hayo yatasaidia kuongezeka kwa miradi ya kitaaluma na kuongeza kasi ya upatikanaji wa udahili na ufadhili wa masomo kwa watanzania.

Alisema GEL imekuwa ikipeleka maelfu ya wanafunzi kusoma vyuo vikuu nje ya nchi na imekuwa ikifuatilia maendeleo yao ya kitaaluma ili kuhakikisha wanahitimu wakiwa na ufaulu unaoridhisha.

Alisema GEL iliamua kuanzisha utaratibu wa kuwatafutia wanafunzi fursa ya elimu nje ya nchi baada ya kubaini kuwa wanafunzi wanaohitaji elimu ya juu nchini ni wengi lakini fursa zimekuwa chache.

Alisema GEL imekuwa ikiwatafutia wanafunzi wakiwemo wa masomo ya uhandisi na udaktari kwenye vyuo mbalimbali vikiwemo vya nchini Ukraine, Uingereza, Marekani, India,Cyprus, China Poland Hungary, Uturuki.

Alisema wanafunzi wengi wanaotaka kusomea fani za uhandisi na udaktari huwa wanakosa nafasi kutokana na ushindani mkubwa kwenye vyuo vya ndani na GEL imekuwa ikiwaunganisha na vyuo vikuu nje ya nchi ambako kunanafasi.

“Wanafunzi wengi hasa wa masomo ya uhandisi na fani za afya kama udaktari huwa wanakosa nafasi kwasababu nafasi zinakuwa chache kwa hapa nchini lakini wanapofika Global Education Link huwa tunahakikisha watoto wote wanapata nafasi ndani ya muda mfupi kwenda kusoma vyuo mbali mbali nje ya nchi,” alisema

Aidha, Mollel alisema mbali na kuunganishwa na vyuo vikuu nje ya nchi kwa harakawanafunzi ambao huwa wanapata changamoto ya ada huwa wanapatiwa mikopo isiyo na riba kwaajili ya ada ili wawahi mwaka wa masomo.

Naye Profesa Mwegoha alishukuru kuwa ushirikiano huo utakuwa na manufaa makubwa kwa chuo hicho kwani wanafunzi wake na wahadhiri watapata fursa ya kwenda kwa muda kwenye vyuo vikuu nje ya nchi.

“Mzumbe ni taasisi kubwa na kongwe hapa nchini kwa kusaini mkataba huu wa ushirikiano tunaona fursa nyingi sana kwa upande wetu ambazo zitatusaidia kitaaluma kwa upande wa wahadhiri wetu na wanafunzi wetu pia,” alisema