Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, ameungana na wananchi wa mkoa huo katika zoezi la kupiga kura mapema oktoba 29,2025, akisisitiza hali ni shwari na ulinzi na usalama imeimarishwa.
Aidha Kunenge ameeleza, wananchi waendelee kujitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba kwa amani na utulivu.

Kunenge amepiga kura katika kituo kilichopo jengo la ofisi ya Mkuu wa mkoa , ambapo alieleza kuwa hali ni shwari na wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi bila usumbufu wowote.
“Hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa, hali ya hewa ni nzuri, na wananchi wanajitokeza kwa utulivu kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema Kunenge.
Alifafanua kuwa vituo vya kupigia kura vimepangwa kwa ukaribu zaidi ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kusafiri umbali mrefu, na kwamba katika baadhi ya maeneo kuna vituo vitatu hadi vinne.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amewahakikishia wananchi kuwa hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yote ya mkoa huo imeimarishwa.

“Kwa siku tatu sasa jeshi la polisi limekuwa mitaani, doria zinaendelea katika kila mtaa ili kuhakikisha wananchi wanapiga kura kwa amani na utulivu, mimi mwenyewe nimetoka kupiga kura, mazingira ni salama ,” alisema Morcase.
Aliongeza kuwa hakuna nafasi ya vitendo vya kihalifu, na wananchi wanaweza kuendelea na shughuli zao za kawaida wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Pwani, Gerald Mbosoli, alisema kuwa vituo vyote 3,941 vilifunguliwa saa 1:00 asubuhi kama ilivyopangwa, na muitikio wa wapiga kura ni wa kuridhisha.

Baadhi ya wananchi akiwemo Maimuna Saidi, Emmanuel Masele, na Fatuma Salehe, walisema wamefurahishwa na utaratibu mzuri wa kupiga kura na kwamba wamepiga kura bila bughudha yoyote.
Emmanuel alieleza kuwa alifika kituoni saa 2:22 asubuhi, akapanga foleni, na baada ya kupewa maelekezo na watendaji husika, alifanikiwa kupiga kura kwa utulivu.







