Na Happy Lazaro, JamhriMedia, Arusha
Halmashauri ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha imepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya zaidi ya shs 75.6 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza kwenye baraza maalumu la bajeti ,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Lucas Kaaya amesema kuwa bajeti hiyo imelenga katika kipaumbele kikubwa cha miundombinu ya barabara ambapo kila kata itapewa shs 10 milioni kwa ajili ya utatuzi wa miundombinu ya barabara.
Kaaya amesema kuwa,changamoto kubwa iliyopo katika wilaya ya Meru ni ubovu wa barabara ndio maana wameamua kuweka kipaumbele katika eneo hilo ili kuondokana na changamoto hiyo ya muda mrefu .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Meru ,Flora Msilu akizungumza kwenye baraza hilo amewataka madiwani hao kuongeza bidii zaidi katika kutafuta miradi zaidi kwenye kata zao ili kuweza kuongeza mapato ya halmashauri .
Nao baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo wakizungumza kwenye baraza hilo, Diwani wa kata ya Kikatiti, Baraka Kaaya amesema kuwa, bajeti hiyo imelenga katika kipaumbele cha barabara ,.maji,elimu na afya na hayo yote wameyawekea mpango mkakati hivyo bajeti hiyo utakidhi mahitaji mengi na itagusa shida za wananchi kwa ujumla .
Kaaya amesema kuwa ,kwa upande wa kata ya kikatiti bajeti hiyo itasaidia kwa kiwango kikubwa sana .
“Kila kata imetengewa bajeti ya milioni 10 kw ajili ya kwenda kutengeneza baranara yale maeneo ambao hayatumiki.kwa muda wote na pia watenga kiasi cha shs 2 milioni kwa ajili ya mafuta ya creda kwa ajili ya kufungua yale maeneo ambayo hafikiki kwa urahisi.”amesema Diwani Kaaya.
Ameongeza kuwa, soko la mnada wa kikatiti wametenga bajeti ya shs milioni 100 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu iliyopo kule ndani kama vyoo na kuboresha soko zima kwani wakina mama wanatandika bidhaa chini hivyo wanatakiwa kutengenezewa mazingira ambayo ni mazuri ambayo yataleta tabasamu kwa wanakinamama .
“Kwa ujumla bajeti ni nzuri na tunamshukuru sana Mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri pamoja na madiwani katika kata zote 26 kwani wameonyesha ushirikiano mkubwa sana kwa ajili ya bajeti hiyo .”amesema .
“Kwa upande wa kata ambayo haijafanikiwa kupata wamewaahidi kwa mwaka mwingine wa fedha unaokuja wataweka nguvu katika maeneo hayo na wanaainisha vipaumbele vyao ndani ya halmashauri ya Meru katika swala zima la barabara, elimu na maji na kule ambapo kuna mapungufu kote watafika .”ameongeza .
Naye Diwani wa kata ya Majengo ,Benard Wilson amesema kuwa bajeti hiyo itatatua kero kubwa ya barabara ambayo imedumu kwa muda mrefu katika kata nyingi za halmashauri hiyo .
Diwani wa kata ya Seela Sing’isi ,Alex Mbise amesema kuwa, bajeti ya mwaka huu imeweka kipaumbele katika utatuzi wa changamoto za barabara katika kata mbalimbali.za halmashauri hiyo ambapo kila kata imepangiwa bajeti ya shs 10 milioni kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo jambo ambalo litaleta manufaa makubwa katika kata na hata wananchi kwa ujumla hasa katika kipindi hiki cha mvua.
“Miradi yote inategemea mapato hiyo tumeweka nguvu katika miradi mbalimbali ili tuweze kupiga hatua zaidi na kuweza kutatua changamoto mbalimbali katika.kata zetu”amesema Mbise.






