Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Shinyanga

HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga imesema kukamilika kwa jengo lake lililogharimu shilingi bilioni tatu kumeboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa halmashari hiyo kwa kiwango kikubwa.

Halmashauri hiyo imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kufanikisha kukamilika kwa ujenzi wa jengo lake pamoja na shule ya sekondari ya Amali Mwambasha iliyoko kwenye halmashauri hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya hiyo, Kalekwa Kasanga wakati akizungumzia mafanikio ya ujenzi wa jengo hilo na namna ulivyosaidia kuboresha kazi zake za kila siku.

Alisema mwaka 2021 walianza kuipokea fedha kutoka serikalini kujenga jengo la halmashauri hiyo ambalo limeshakamilika kuanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 16.4.2025.

“Kwa dhati kabisa tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kupata jengo hili kubwa ambalo lina ofisi nyingi za kutosha na linatumika na wafanyakazi wote 130 wa halmashauri kutoka idara 20,” alisema

“ Kwa kweli utendaji wa kazi umeboreka kutokana na kukamilika kwa jengo hili kwasababu hakuna kubanana tena lakini pia kwa kupatikana kwa ofisi za kutosha halmashauri sasa tunaweza kuhudumia watumishi wengine 2,450 wanaotoka kwenye zahanati, vituo vya afya, shule, vijiji na kata zote 26 za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,” alisema.

Aidha, alisema tangu halmashauri hiyo imeanzishwa ilikuwa na ofisi zake katika Manispaa ya Shinyanga eneo la Chamagoha na mwaka 2019 maelekezo yalitoka kwa halmashauri zote za wilaya ziende kuanzisha ofisi maeneo ambako wananchi wake wanaishi ambako ndiko maeneo yake ya kiutawala.

“Kwa hiyo kama zilivyo halmashauri zingine halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ilitekeleza maelekezo ya serikali na kuhamishia ofisi zake katika kijiji cha Isilamagazi tarafa ya Nindu na hatukuwa na jengo tulitumia ofisi za taasisi ya World Vision ambao walikuwa wamemaliza kazi zao ilikuwa kama nyumba,” alisema

“Tulihamia hapo na watumishi wetu 130 na mwaka 2021 tulianza kupokea fedha kutoka serikalini tukaanza kujenga jengo hilo tulipokea bilioni tatu na kulikamilisha na tukahamia tarehe 16.4.2025 tunamshukuru Rais Samia kwa kutuwezesha kupata jengo kubwa,” alisema

“Namshukuru Mungu sana katika ukamilishaji wa hili jengo na pia serikali hii inayoongozwa na Rais Samia kwa kuziwezesha halmashauri kuwa na majengo yake, kwasababu mtu yeyote ili afanye kazi lazima awe kwenye mazingira mazuri kwa hiyo jengo hili ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali kujenga mazingira wezeshi kwa watu wake ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi wake,” alisema.

Wakati huo huo aliipongeza serikali kwa kuhakikisha shule ya sekondari ya amali Mwambasha iliyoko kwenye halmashauri hiyo imekamilika.

Alisema kukamilika kwa shule hiyo kunatoa fursa kwa elimu ya vitendo katika Mkoa wa Shinyanga.