Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chama cha Alliance Democratic Change (ADC), kimemtangaza Willison Elias kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali ya Willison, chama hicho pia kimemteua mwanasiasa mkongwe Hamad Rashid Mohamed kuwa mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Wagombea hao wamepitishwa mwishoni mwa wiki na mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa chama hicho, Shabani Itutu, amesema wagombea hao hawakuwa na upinzani, hivyo kupitishwa rasmi.

“Nafasi hizi hazikuwa na wagombea wengine zaidi ya hawa wawili tu…kama mnavyojua chama chetu kinafuata demokrasia, tumeona ni vema tuitishe mkutano mkuu maalumu ufanye uamuzi, hakuna haja ya uchaguzi, tunafuata demokrasia,” amesema.
Amesema chama hicho kina ilani inayogusa maisha ya watu, kwa sababu wanaamini afya ni jambo muhimu, hivyo wakipata fursa ya kuongoza nchi kila mwananchi atapata haki ya kutibiwa bure.
“Tunafanya hivi kwa sababu tunaamini wananchi wetu uwezo wao ni mdogo wanahitaji msaada, ndiyo maana utakuta wanaishi na wagonjwa majumbani hawana uwezo wa kuwatibia,” amesema.

Amesema elimu na afya vitakuwa bure, kwa sababu uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo ndani zina uwezo wa kuhudumia wananchi.
Amesema wakifanikiwa kushika madaraka watahakikisha mama lishe na wamachinga wanafanya biashara kwa uhuru, kwa kuwajengea jengo lao katikati ya Jiji la Dar es Salaam, Bajaji na pikipiki zitaondolewa ushuru.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Maridhiano, Sheikh Alhad Musa Salum, amesema chama hicho ni sahihi kwa sababu kinajali masilahi mapana ya taifa zima.
“Vyama vyote vitambue amani ni nguzo kubwa kwa taifa, kwa sababu uchaguzi utapita, Tanzania itabaki.
“Nawaombeni mnapohubiri muwe mnahubiri Amani, tunaamini uwepo wako Hamad Rashid katika chama hiki tunaamini utapeperusha bendera yetu vema katika Uchaguzi Mkuu,” amesema.
Hamad Rashid amesema kuwa kama atapata ridhaa ya wananchi kuwa rais, atahakikisha Zanzibar inajimudu kwa chakula, tofauti na sasa, na pembejeo zitakuwa ni bure.
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inasisitiza kuzingatia sheria za nchi, ikiwamo sheria za uchaguzi na vyama vya siasa ili kufanya Uchaguzi Mkuu kuwa huru na wa amani, kwa kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.