Na Dk. Reubeni Lumbagala, JamhuriMedia, Tanga
Elimu ni gharama. Elimu ina mahitaji mengi ambayo yanahitaji fedha ili kuyakamilisha ili kupata utulivu wa kujifunza darasani. Serikali inasimamia na kutekeleza kikamilifu Sera ya Elimumsingi bila ada ambapo hutumia fedha nyingi kuwezesha upatikanaji wa mahitaji muhimu shuleni ili shughuli za ufundishaji na ujifunzaji ziweze kufanyika vizuri na kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi gharama za kusomesha watoto wao.
Kupitia Sera ya Elimumsingi Bila Ada, fedha zinawafikia walengwa ipasavyo. Serikali hutuma fedha moja kwa moja katika akaunti za benki za shule ili zigharimie masuala mbalimbali ya kuendesha shule kama vile shughuli za utawala, taaluma, mitihani, ukarabati, michezo na mahitaji mengine kadha wa kadha.
Sambamba na hilo, serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosoma Stashahada kwa kozi za kipaumbele, Shahada ya kwanza na kuendelea katika kozi mbalimbali ili kwa pamoja vijana wa Kitanzania waweze kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika shule za msingi na sekondari, hasa uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya kujifunza pamoja na uwepo wa walimu mahiri, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya kati na taasisi za elimu ya juu imeongezeka sana huku wengi wakiwa na sifa ya kupata mikopo hiyo.
Ikumbukwe kuwa kadri idadi ya waombaji mikopo inavyoongezeka ndivyo mahitaji ya fedha za mikopo yanavyoongezeka pia. Ili kuendana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga vyuo vya kati na juu, HESLB imechukua hatua ya kuunganisha nguvu kati ya sekta ya umma na binafsi (Public and Private Partnership – PPP) ili kutafuta vyanzo vingine vya fedha au wafadhili nje na serikali kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata mikopo hiyo.
Katikati ya mahitaji makubwa ya fedha ya kugharamia elimu ya kati na ya juu, PPP haikwepeki, ni muhimu sana. Kimsingi, HESLB imeanzisha mashirikiano na taasisi za umma na binafsi zenye uwezo wa kufadhili wanafunzi ili wanafunzi wengi zaidi wapate mikopo. Lengo ni baadhi ya wanafunzi kupata mikopo kupitia HESLB na wengine wapate kupitia taasisi nyingine zenye kutoa ufadhili wa elimu, ili hatimaye kuwepo na kundi kubwa linalonufaika na ufadhili kukidhi mahitaji yaliyopo.
Mnamo Oktoba 2025, HESLB ilisaini makubaliano na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambapo NCAA imetoa ufadhili kwa wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni kutoka jamii zinazozunguka Hifadhi ya Ngorongoro.
Kamishna Mkuu wa NCAA, Abdul-Razaq Badru amesema “Tutaanza kwa kuwafadhili jumla ya wanafunzi 50 watakaodahiliwa kwenye fani za Sayansi ya Anga, Mali Kale na Akiolojia pamoja na Uhifadhi wa Wanyamapori.”
Januari 29, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, alifanya ziara Jijini Arusha kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Compassion International Tanzania (CIT) ikiwa ni jitihada za HESLB kuongeza vyanzo mbadala vya ufadhili (alternative financing).
Katika ziara hiyo, HESLB na CIT walisaini tamko la nia ya kushirikiana (Statement of Intention to Collaborate) ili kuwatambua wanafunzi wanaotoka mazingira magumu ili wapate kipaumbele katika upangaji wa mikopo. Jambo hili ni jema sana.
Kama hiyo haitoshi, Machi 26, 2026, HESLB ilifanya kikaokazi na taasisi 205 zilizosajiliwa na HESLB na zinazotoa ufadhili wa wanafunzi kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kwani taasisi hizo zina mchango mkubwa katika kutanua wigo wa wanufaika wa mikopo ya elimu nchini. Kikaokazi hicho kilifanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) Jijini Arusha.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Kiwia amesema kikao hicho ni muhimu na kina lengo la kuboresha ufanisi wa utendajikazi na kuongeza wigo wa wanafunzi wanaofadhiliwa na taasisi hizo huku akiishukuru serikali kwa kutoa shilingi trilioni 3.6 kugharamia mikopo ya elimu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kwa kumalizia, ni vyema watu binafsi, taasisi za dini na mashirika mbalimbali wajitokeze kuiunga mkono HESLB kufadhili wanafunzi ili wanafunzi wengi zaidi wapate mikopo badala ya kuiachia serikali pekee jukumu la kutoa mikopo ya elimu ya kati na juu. Nakumbuka Machi 14, 2026, HESLB iliandaa futari maalum katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam. Katika futari hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Prof. Hamisi Dihenga, alitoa wito kwa wadau kujitokeza kutoa ufadhili wa masomo (Scholarship).
“Nia yetu ni kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika juhudi za kuimarisha elimu ya juu nchini. Tupo tayari kushirikiana na wadau wengine kama ambavyo kumeshakubaliana na NCAA ambao wao watafadhili wanafunzi 50 wa vyuo vikuu, tunaomba wadau wengine pia wajitokeze tuwasaidie vijana wetu,” amesema Prof. Dihenga. Kiukweli, ongezeko kubwa la wanafunzi vyuoni, linahitaji PPP kuweza kukidhi mahitaji makubwa ya fedha yaliyopo kugharamia masomo. Wadau jitokezeni, bila hivyo hatutoboi aisee.
Maoni: 0620 800 462






