
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, WAKATI WA KUFUNGUA RASMI BUNGE LA 13 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, TAREHE 14 NOVEMBA 2025
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika;
Naanza na wingi wa shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo. Kwa mujibu wa Ibara ya 91, Ibara ndogo ya kwanza, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana dhima ya kulifungua rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni kwa msingi huo, leo nipo hapa kulihutubia Bunge ili kutimiza matakwa ya Ibara hiyo ya Katiba.
Kabla ya kufanya hivyo, nianze na jambo la huzuni lililotokea hapa nchini. Niwaombe tusimame kwa dakika moja kuomboleza na kuwaombea ndugu zetu waliopoteza maisha katika vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu tarehe 29/10/2025.
Mimi binafsi nimehuzunishwa sana na tukio lile. Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, na tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Aidha, kwa majeruhi tunawaombea wapone kwa haraka, na kwa wale waliopoteza mali zao tunawaomba wawe na stahamala na uvumilivu. Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea (Enquiry Commission) ili tujuwe kiini cha tatizo. Taarifa hio itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kueleza sononeko hilo, nijielekeze sasa kukupongeza wewe Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilala na kwa kupata imani ya Waheshimiwa Wabunge waliokuchagua kuwa Spika wa Bunge hili la 13. Ni imani yangu kuwa uzoefu wako katika Bunge hili utakuongoza kusimamia utekelezaji wa shughuli za Bunge kwa ufanisi mkubwa. Aidha, nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Spika Mstaafu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuliongoza vyema Bunge la 12. Serikali inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu ya Bunge hili la 13.
Kwa kauli hiyohiyo, nimpongeze pia Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge hili.
Aidha, nirejee pongezi zangu kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemb, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameapishwa leo asubuhi.
Niwapongeze pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuaminiwa na Watanzania kuwawakilisha, katika kazi adhimu ya kutunga sheria, kuishauri na kuisimamia Serikali kupitia Bunge hili la 13. Waheshimiwa Wabunge, Hii ni dhamana na dhima kubwa sana mliyopewa na wananchi, na vivo hivyo, matarajio ya wananchi kwenu ni makubwa pia. Matarajio yao ni kuwa mtatumia muda wenu mwingi kuwa na mijadala inayoakisi raha na karaha wanazoziona, na mtaisimamia na kuishauri Serikali ipasavyo juu ya kutatua changamoto zao, na kwamba wakati wote mtajielekeza kulinda maslahi ya wananchi waliowachagua, na maslahi mapana ya Taifa.
Mheshimiwa Spika;
Kwa vigezo vyovyote vile, Bunge hili ni jipya. Takwimu zinaonesha kuwa Wabunge 223 kati ya Wabunge 393, sawa na asilimia 56.7 ni Wabunge wapya kabisa. Aidha, asilimia 40.5 ya Wabunge wote ni Wanawake. Wabunge Wanawake waliogombea majimboni safari hii ni 36 ikilinganishwa na Wabunge 21 katika Bunge lililopita. Takwimu hizi zinatueleza kuwa Uchaguzi Mkuu umeleta mabadiliko makubwa kwa kuongezeka kwa idadi ya Wabunge Wanawake walioshinda kupitia majimbo; na kuongeza idadi ya Wabunge Wanawake wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Spika,
Uchaguzi Mkuu wa kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano; Rais wa Zanzibar; Wabunge; Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi; na Madiwani ulifanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 nchini kote. Watanzania kwa mamilioni walijitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi waliowataka. Kazi iliyo mbele yetu sasa ni kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa, ili sote kwa pamoja tuijenge, tuitunze na tuilinde nchi yetu, na kuzidi kunyanyua hadhi ya Taifa letu.
Nitumie nafasi hii kuwashukuru tena wananchi wa Tanzania kwa kujitokeza na kushiriki vyema kwenye hatua zote, kuanzia kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura; kuhakiki daftari na kupiga kura. Kwa mara nyengine tena wananchi wamethibitisha kuwa kushiriki uchaguzi ndio njia ya uhakika na ya salama ya kubadilisha viongozi wasioridhika na au wasioridhika na huduma zao. Njia nyingine zozote hazina kheri wala salama ndani yake.
Niendelee kuipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuendesha vyema Uchaguzi Mkuu wa kwanza tangu kuundwa upya kwa Tume hiyo. Safari hii Wakurugenzi wa Halmashauri hawakusimamia uchaguzi, wala hakuna Mgombea aliyepita bila kupingwa. Sisi tuliogombea na vyama vyetu, hatukukosa viwanja vya kufanyia mikutano. Kwa ujumla, kampeni zilikwenda vyema. Aidha, utaratibu uliofanyika wa kuongeza vituo vya kupigia kura ulisaidia sana kuondoa msongamano katika vituo hivyo. Kwa hakika, upigaji wa kura ulirahisishwa sana na haukuchukua muda mwingi wa wananchi kama ilivyozoeleka. Jambo hili limewafanya baadhi ya waangalizi wa uchaguzi kudhani kwamba wananchi hawakujitokeza kupiga kura.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuwa uchaguzi ulifanyika, kulijitokeza vurugu na uvunjifu wa amani ambao ulisababisha uharibifu wa mali, kupoteza maisha na kuhatarisha usalama wa Nchi. Tunapoenda mbele, niwasihi sana Watanzania tuongozwe na dhamira ya maelewano, ushirikishwaji, kujirekebisha, na umoja.
Kwa wanangu, vijana wa taifa hili la Tanzania, niseme kuwa Nchi hii imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa. Sisi wazazi wenu tungeshawishika kuyafanya mliyoyafanya wakati huu, nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona leo. Niwasihi sana wanangu, nchi hii ni yenu, kwa shida zozote zile zinazowakabili, msikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe. Msikubali kukata tawi la mti ambalo mmeukalia. Hili nawaomba mlikatae kwa nguvu zenu zote. Ninyi ndio walinzi na wajenzi wa Taifa hili, nawasihi kamwe msije kuwa Wabomoaji wa Taifa lenu.
Kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki, ninatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya. Nikiwa Mama na Mlezi wa Taifa hili, ninavielekeza vyombo vya sheria na hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao.
Ninatoa msamaha huo kwa sababu, hata maneno ya Mungu katika Kitabu cha LUKA sura ya 23 Mstari wa 34 yanasema, na hapa nanukuu: “Yesu akasema, Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.”
Ndugu zangu Watanzania, tujifunze kutokana na mapito yetu, hapana shaka kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, ila, demokrasia kamili inaweza kutafsiriwa kwenye mitazamo tofauti (haina formula moja). Kama Taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha. Hivyo basi, sote kwa umoja wetu tunapaswa tuitumie fursa hii tuendelee kujifunza, tujirekebishe na tukubaliane jinsi ya kuiendesha nchi yetu kidemokrasia kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi zetu na sio za kuletewa. Kama tulivyoagizwa na Ilani ya CCM ya mwaka 2025 hadi 2030, moja ya hatua itakayotufikisha kwenye maelewano hayo ni marekebisho ya Katiba yetu. Serikali imeahidi kuanza kulifanyia kazi suala la mabadiliko ya Katiba ndani ya siku mia za muhula wa pili wa Awamu ya Sita kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maelewano.
Mheshimiwa Spika;
Tunapozungumzia umoja wa Kitaifa tunaongozwa na uwepo wa Tunu ya Muungano wetu. Hivyo basi, kuudumisha kuimarisha na kuuenzi Muungano wetu kutaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali tunayoiunda. Tutaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha tunatatua changamoto za Muungano kila zinapojitokeza.
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya sita iliendeleza tuliyoyaanza katika awamu wa tano, na hivyo kaulimbiu yake ilikuwa ‘Kazi Iendelee’. Ninyi ni mashahidi kuwa kazi iliendelezwa na mengi yalikamilishwa, kama nilivyoeleza katika hotuba ya kufunga Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 Juni mwaka huu 2025. Niwahakikishie katika miaka mitano ijayo tutalinda na kuendeleza mafanikio haya pamoja na kuleta mafanikio mengine na makubwa zaidi.
Katika kipindi cha Kampeni, mimi na Mgombea Mwenza tulitembea nchi yote kuomba kura, na tulisikiliza na kuyabeba matakwa na mahitaji ya wananchi katika kuijenga nchi yetu kwa maisha bora zaidi ya baadae. Tuliwaahidi kuwa, wakitupa tena dhamana ya kuongoza Taifa letu, tutajielekeza katika kutekeleza kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’. Yaani, kuhakikisha kuwa jitihada zozote tunazozichukua za kuleta maendeleo, zitalenga kuinua na kuongeza thamani ya utu wa watu wetu wa Tanzania. Hakika tulisikiliza na kuelewa matamanio ya wananchi ya kupata Serikali inayoshughulikia changamoto zao, kama vile; suala la gharama za maisha, kuongeza fursa za kazi na ajira ili waweze kujiendeleza kiuchumi; na kuimarisha ustawi wa jamii zetu. Nataka niwahakikishie kwamba Serikali itachochea upatikanaji wa fursa za kiuchumi na kujenga matumaini kwa vijana, Wanawake, makundi ya wenye ulemavu, na hata wazee kuanzia mijini mpaka vijijini.
Mheshimiwa Spika;
Nianze na masuala ambayo niliwaahidi wananchi kuwa tutaanza nayo ndani ya siku 100 za mwanzo za kazi. Kwanza kabisa linahusu utumishi na utawala bora, nalo ni suala la uundwaji wa Serikali. Niliwaahidi wananchi kuwa Serikali nitakayoiunda itawajibika na kuendelea na mageuzi ya sera zinazogusa maslahi na ustawi wa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Hivyo basi, ni lazima viongozi wa Serikali kwa ngazi zote, kuanzia Mawaziri hadi Maafisa Tarafa, wawe karibu na wananchi ili kuweza kufahamu changamoto zao na kuwajibika kwao. Kwa kuwa ahadi tulizotoa ni nyingi, matamanio ni mengi, matarajio ni makubwa, na muda wa kuyatimiza haya ni mchache, tutaongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya Serikali ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea. Nayasema haya mapema kwa watendaji waliopo Serikalini, wakiwemo Makatibu Wakuu, na wale nitakaowateua kwa ajili ya kujitayarisha kisaikolojia na kujipanga vyema kufanikisha malengo hayo. Wananchi wanahitaji mabadiliko chanya kwa maendeleo. Watendaji msipobadilika, kuendana na matarajio ya wananchi, tutawabadilikia!
Mheshimiwa Spika;
Katika hotuba ya kufungua Kampeni tarehe 28/08/2025 nilitaja mambo ambayo Serikali ingeanza nayo ndani ya siku 100 za kazi.
Tuliahidi kutoa ajira kwa fani za Sekta ya Afya na Elimu. Leo ikiwa ni siku ya kumi na mbili tangu muhula huu wa pili wa Awamu ya Sita uanze, tayari tumeshatangaza nafasi za ajira 7,000 za walimu na nafasi za ajira 5,000 za watumishi wa afya. Hatua hii ni ya mwanzo kujibu kiu ya wananchi ya kuboresha huduma za afya na elimu.
Katika hatua nyingine, tunajiandaa kuanza kwa majaribio ya Bima ya Afya kwa Wote. Serikali itakuja kwenu Waheshimiwa Wabunge na mapendekezo ya namna ya kufanikisha majaribio hayo, na niwaombe muunge mkono mapendekezo hayo ambayo yatakuwa mwanzo wa mageuzi katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote nchini. Tunadhamiria pia kuviunganisha vituo vya huduma za afya kidijitali na kuhakikisha vinakuwa na vifaa na huduma za viwango stahiki kwa kila ngazi husika. Tunakusudia kuweka viwango vinavyofanana ili watumiaji wa bima ya afya mijini na vijijini wawe na huduma zinazolingana.
Katika hatua nyengine, nimeshaielekeza Wizara ya Afya kusimamia maelekezo ya kutozuiwa maiti kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, wakati familia zikiendelea na taratibu za kulipa deni la matibabu kwa njia zinazolinda utu wao. Niseme kwamba, ni kupitia mpango huu wa bima ya afya, kadhia hii inakwenda kukomeshwa. Kwa sababu gharama za matibabu zitalipwa na bima ya anayetibiwa. Niwasihi wananchi wote kuweka kipaumbele kwa afya zetu, kwa kila mmoja wetu kuwa na bima ya afya pamoja na wanaomtegemea.
Mheshimiwa Spika;
Ilani ya CCM ya 2025-2030 imeahidi na mimi nilitangaza ahadi hiyo kuwa nitaunda Tume ya kuanzisha Mazungumzo ya Maridhiano na Upatanishi na kuandaa mazingira ya kuanza kwa Mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hata hivyo, kutokana na uvunjifu wa amani uliotokea nchini, tunahitaji kufanya tathmini ya kina ili tujue kiini na sababu ya kadhia hiyo, na ndipo tuunde Tume ya Maridhiano.
Katika Muhula kwa kwanza wa Awamu ya sita tulikuja na falsafa ya R4 ili kuliunganisha Taifa. Serikali ilionesha utayari wakati wote kuleta maridhiano, ili kwa pamoja tuweze kulijenga na kulitunza Taifa letu. Serikali ilinyoosha mkono kuwavuta na kuwakaribisha Vyama vya Siasa, Vyama vya Kijamii, Sekta binafsi na hata Jumuiya za Kimataifa, ili kwa pamoja tuijenge Tanzania. Waheshimiwa Wabunge, mkono huo wa urahimu ulileta matumaini kwa nchi, kabla ya baadhi ya wadau kuamua kuuachilia au Kuuputa mkono huo. Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano, ili kwa pamoja tujenge mazingira muafaka kwa maendeleo ya Taifa letu. Tutajifunza kutokana na makosa na mapungufu ya taasisi zetu za kidemokrasia. Tanzania inauzoefu wa miongo mingi ya demokrasia na amani. Tanzania ina Demokrasia iliyokomaa hata hivyo tutaendelea kuiboresha kulingana na mazingira na wakati. Ni jukumu letu sasa kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wa Nchi hii ni Vijana, tutaweka kipaumbele kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii, na kuwajengea kesho iliyo bora zaidi.
Ili kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika kujenga mustakabali mwema wa Taifa letu, tutaweka kipaumbele kwenye ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya Maendeleo yao. Natambua kumekuwa na majukwaa mengi ya kuwafikia vijana ila bado shughuli zao zinafifishwa na masuala ya kisiasa, na majukwaa hayo kupoteza malengo na mvuto kwa vijana. Mimi na wenzangu tumefikiria kuwa na Wizara kamili itakayoshughulika na mambo ya vijana, badala ya kuwa na Idara ndani ya Wizara yenye mambo mengi. Vile vile, ninafikiria kuwa Washauri wa masuala ya vijana ndani ya Ofisi yangu.
Jambo jengine tuliloahidi kulitekeleza ndani ya siku 100 za awali za kazi ni kuchukua hatua za kuongeza mitaji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za Vijana na Wanawake kwa kutenga shilingi bilioni 200. Serikali inaendelea kuangalia njia nzuri ya kuimarisha mfuko huo kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa walengwa. Aidha, kwa kushirikiana na sekta binafsi, tutaanzisha madirisha ya uwekezaji kwa Vijana (Youth Investment Windows). Madirisha haya yatatoa mikopo nafuu na mitaji ya uwekezaji kwa biashara za vijana.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na hayo niliyoyaeleza, kuna mengi zaidi ambayo tumejipanga kuyafanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ni dhima ya Serikali kuendeleza ukuaji wa Uchumi. Katika kipindi hiki tutaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 hadi 2050, tukilenga kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea. Dira mpya imeweka vigezo vya kuchagua sekta na maeneo ya kupewa kipaumbele yaliyobainishwa kwenye andiko la Dira yenyewe. Kati ya mikakati itakayofanyiwa kazi ni kuwekeza zaidi kwenye sekta zinazoajiri watu wengi na miongoni mwa sekta hizo ni kilimo, utalii, viwanda, ujenzi na madini.
Malengo yetu ya kiuchumi ni kupandisha kasi ya ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.6 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 7 kuelekea mwaka 2030. Ukuaji huu utaiwezesha Serikali kuboresha huduma za kijamii na kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi. Tutaimarisha masoko ya mitaji kwa kuhamasisha uwekezaji wa ndani, na kutumia rasilimali zetu kama madini kudhamini mikopo ya uwekezaji, badala ya kuweka mzigo mkubwa kwenye Deni la Taifa. Mwelekeo wetu ni kukua kwa pamoja kwa uchumi unaogusa maisha ya mtu mmoja mmoja (Micro economy) na uchumi jumla (Macro economy).
Mheshimiwa Spika;
Mtakubaliana nami kuwa Sekta Binafsi ni nguzo muhimu ya ukuzaji wa uchumi, hususan Sekta Binafsi ya ndani. Tutaboresha zaidi mazingira ya biashara nchini kwa kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI). Aidha, tutatekeleza mapendekezo ya Tume niliyoiunda ya Kuboresha Mifumo ya Kodi nchini ili kuwapatia wafanyabiashara wetu wepesi katika kufanya biashara zao.
Tutaendelea kuweka nguvu zaidi kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa ambayo ni hatua muhimu katika kupunguza gharama za maisha kwa Wananchi. Pia tutaweka motisha kwa viwanda vya ndani ili viweze kuzalisha kwa gharama nafuu na kuuza kwenye soko la ndani na nje. Tutaongeza vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuchochea uzalishaji na kukuza ushindani wa bidhaa za ndani.
Mbali na mikopo, tutafungua fursa mahsusi kuhamasisha vijana na wamiliki wa biashara ndogo kupata elimu ya biashara na kuweza kujisajili katika Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Serikali (TANSIS).
Vile vile, kupitia vyuo vyetu vya ufundi stadi VETA tutaongeza programu maalum za mafunzo ya ufundi stadi na kuunganisha programu hizi na miradi ya mikakati kama reli ya kisasa (SGR), uendelezaji wa bandari, uchumi wa buluu, madini na gesi ili vijana hawa wapate uzoefu na waweze kuajirika. Serikali itaanzisha Kanda za Kuendeleza Ujuzi zitakazowawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika makampuni ya sekta binafsi, na kuangalia uwezekano wa kutoa vivutio maalum kwa makampuni yatakayotoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana. Aidha, tutaweka mazingira ya kuhakikisha tunakuza vijana kwenye uongozi kwa kuwezesha vyuo vyetu kufanya mafunzo ya ulezi na ukuzaji wa vijana viongozi (mentorship).
Tutataizama mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya Halmashauri zetu ili kuboresha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa walengwa. Vile vile, ni vyema walengwa wakajua kwamba Fedha hizi ni mkopo na sio msaada, ni mbegu na sio mavuno na ni mtaji na sio ruzuku, hivyo marejesho na tija yake lazima ionekane. Matamanio yangu ni kuona ifikapo mwaka 2030, tuwe tumetengeneza wawekezaji vijana ambao watatoa ajira kwa vijana wenzao.
Kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo tutahamasisha ufadhili kwa biashara za wanawake, Ili kuwasaidia wanawake wanaofanya kazi kwenye masoko, tutaongeza na kuratibu kwa karibu Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kurasimisha biashara zao na kuwawezesha kukopesheka. Tutawekeza katika kuboresha miundombinu ya masoko, mifumo ya maji safi na maji taka, huduma za afya, na vituo vya matunzo ya watoto kwenye masoko.
Katika hatua nyingine, tutalipa kipaumbele suala la kutenga maeneo ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ili Serikali iwatambue na kuwarasimisha ili waweze kufanya kazi zao bila bughudha na wachangie kwenye Pato la Taifa. Kwa rasilimali ambazo nchi yetu imebarikiwa na nguvu kazi kubwa tuliyonayo, ninaamini tunaweza kabisa kujipanga na kufikia lengo hilo. Kwa kufanya hivyo, ndio tutafikia lengo letu la kuzalisha ajira milioni 8.5 katika sekta mbalimbali ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa huduma za kijamii, maendeleo makubwa yamepatikana kwenye sekta ya maji, ambapo hali ya upatikanaji wa maji ilipanda kutoka asilimia 84 hadi asilimia 91.6 mijini, na kutoka asilimia 70.1 hadi asilimia 85 vijijini. Tumefika pazuri kuliko pale tulipokuwa mwaka 2021. Hata hivyo, azma ya Serikali ni kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa maji safi, salama na uhakika. Hivyo tunakwenda kuongeza nguvu ili kuyafikia yale maeneo machache ambayo upatikanaji wa maji bado ni changamoto.
Katika miaka 5 ijayo, tutakamilisha ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji ambayo itategemea maji kutoka Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Tutakamilisha miradi mikubwa ya maji inayoendelea ikiwemo miradi ya maji ya miji 28, na miradi mikubwa ya bwawa la Kiwira (itakayohudumia Mbeya), bwawa la Kidunda, Bonde la Mto Rufiji (itakayohudumia Dar es Salaam, Lindi na Pwani), Same-Mwanga-Korogwe (itakayohudumia Kilimanjaro na Tanga), na upanuzi wa Capri Point (itakayohudumia Mwanza), kwa kuitaja kwa uchache.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye sekta ya afya, mbali na masuala ya Bima ya Afya kwa Wote, na ongezeko la ajira za watumishi wa afya ambayo nimeshayagusia, tutakamilisha ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati zinazojengwa kote Nchini. Tutaendelea kuboresha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuongeza uwezo wake kutoka vitanda 1,435 vya sasa hadi vitanda 1,757 ifikapo 2030. Itakapokamilika, itaweza kutoa huduma za kibingwa na kuwa hospitali ya kutumainiwa na kukimbiliwa katika Afrika ya Mashariki.
Tutaongeza huduma za kibingwa za afya kwenye hospitali zetu za rufaa za Mikoa na hospitali za rufaa za Kanda, ili tuwapunguzie gharama wananchi kutafuta huduma za rufaa nje ya Mikoa yao. Tunataka, badala ya kuwa na watu kuzifuata huduma, huduma ziwafuate watu.
Tutaendelea kuwekeza katika kujenga uwezo wetu wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Tumejipanga kujenga hospitali kubwa ya Kitaifa ya magonjwa ya mlipuko na tutaijenga Mkoani Kagera.
Vilevile, tutajielekeza katika kuongeza uwezo wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kupunguza uagizaji na kupunguza gharama za matibabu. Katika hili, tutavihakikishia viwanda vya ndani soko la uhakika kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
Halikadhalika, tutakuza utafiti, utambuzi na utoaji wa ithibati wa dawa zetu za asili. Baada ya uwekezaji huu tutajielekeza zaidi kwenye kinga (preventive medicine) tofauti na sasa ambapo tumejikita zaidi kwenye tiba (curative medicine) pekee.
Aidha Serikali inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za afya na ahadi yetu ni kuendeleza ushirikiano huu.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Elimu, katika miaka mitano ijayo tunaanza utekelezaji kamili wa maboresho ya Sera ya Elimu inayosisitiza elimu ujuzi. Tutaendelea kuweka mkazo zaidi kwenye masomo ya sayansi na hisabati (STEM). Azma yetu ni kuongeza wanasayansi wabobezi katika eneo la sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia za viwanda. Tutatumia Mfuko wa Samia Scholarship kusomesha wanasayansi hawa ndani na nje ya nchi. Jambo hili litakwenda sambamba na kukamilisha shule maalum za Sekondari za Wasichana za Sayansi na zile za vipaji za Wavulana katika kila mkoa. Ili kuhakikisha mitaala na silabasi zetu zinatekelezwa kikamilifu, tutaunganisha kwa njia ya kidijiti shule za vijijini na mijini ili kubadilishana uzoefu na taarifa.
Kama tulivyowaahidi wananchi, tutaongeza mikopo ya elimu ya juu, kwani kipindi hiki kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tutakuwa na kampasi za vyuo vikuu kila mkoa. Vilevile, tutasimamia mpango wetu wa kuhakikisha kila Wilaya ina chuo cha VETA chenye vifaa stahiki vya mafunzo kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika;
Nilishagusia suala la kuongeza walimu. Pamoja na walimu, tunaenda kuwekeza zaidi pia kwenye miundombinu ya shule za awali, msingi na sekondari mpya pamoja na kuongeza madarasa kwenye shule zilizopo.
Tunapotekeleza maendeleo jumuishi, tutaendeleza jitihada tulizizianza za kuweka miundombinu na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum; pamoja na hao, tutaendeleza fursa muhimu ya kuwasomesha na kujiendeleza kwa watoto wenye magojwa adimu (rare diseases) wanaohudumiwa majumbani.
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano ijayo, tunaenda kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta za uzalishaji, tukianza na kilimo. Tutaongozwa na dhana ya “Kilimo ni Biashara, Mkulima ni Mwekezaji“. Lengo letu ni kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hii kutoka asilimia 4 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Kwa kufanya hivyo, tunalenga sio tu kujihakikishia utoshelevu wa chakula, bali pia tutawekeza kwenye mnyororo wa thamani ili kuwanufaisha Watanzania wengi walioajiriwa kwenye sekta hii. Tunakusudia kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya mahindi, mchele na mbogamboga (Horticulture), barani Africa.
Tutafanya hivyo kwa kujielekeza kwenye kilimo cha kisasa kwa kuongeza pembejeo kama mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa ruzuku, tutaongeza upatikanaji wa maji ya uhakika na kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka ekari milioni 3.4 hadi ekari milioni 5, kwa kukamilisha ujenzi wa mabwawa na skimu za umwagiliaji zinazoendelea na kuanzisha skimu mpya ikiwemo kwenye bonde la Mto Rufiji. Aidha, tutaanzisha vituo vya ukodishaji zana za kilimo, ambavyo vitatoa huduma za matumizi ya teknolojia katika kilimo chetu. Ili kukuza uwekezaji kwenye sekta ya Kilimo, tutaziimarisha benki zetu za Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Ushirika ili zichochee mapinduzi tunayoyatazamia.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuongeza uzalishaji, lazima pia tudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno (post harvest loss). Hivyo, tutaendelea kuwekeza katika kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Aidha, tutazidi kuboresha mifumo ya stakabadhi ghalani ambayo imeshaanza kuwaletea manufaa wakulima wa mazao mbalimbali yaliyojumuishwa kwenye mfumo huo. Katika kupanua masoko yetu nje, na kutumia fursa za diplomasia yetu ya uchumi kuyatumia masoko ambayo tayari tulishafungua, tutahakikisha kuwa fursa hizi zinakuwa na makubaliano yanayotekelezeka ili kuwa na uhakika wa masoko haya. Hapa tunakusudia masoko ya mbaazi, choroko na ufuta, kupata masoko ya uhakika.
Pamoja na kujitosheleza kwa chakula kwa 128% kwa sasa, mwelekeo wetu ni kuendelea kupiga hatua kwenye uzalishaji wa sukari na mafuta ya kupikia hususan uzalishaji na usindikaji wa alizeti, chikichi na ufuta.
Mheshimiwa Spika;
Kuna mazao ya biashara ambayo yalikuwa yakifanya vizuri sana na kuwanufaisha wakulima wengi, lakini yameathiriwa na ama bei za soko duniani, au wawekezaji waliopewa viwanda vya kuchakata mazao hayo kushindwa kuviendesha vyema viwanda hivyo. Tutayasimamia kwa karibu zaidi mazao ya Chai, Kahawa, Parachichi na Pamba tukiwa na shabaha ya kupanua masoko, kuongeza ushindani wa bei na kuwafaidisha zaidi wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika;
Serikali imeanza kuona fursa na kuleta mageuzi kwa sekta ya Ufugaji. Miongoni mwa ahadi zetu kubwa ni kuongeza eneo lililopimwa na kutengwa kwa shughuli za ufugaji kutoka ekari milioni 3.46 hadi ekari milioni 6. Hatua hii itaepusha migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, na itaongeza wigo wa uzalishaji wa malisho ya mifugo ili tuelekee kwenye ufugaji wa kisasa. Katika hatua za kuyafungua masoko ya kimataifa, tutaendeleza Chanjo, pamoja na Utambuzi wa mifugo yetu nchini, ili kuongeza ubora wa mazao ya mifugo, tuweze kuingia kwenye kumbukumbu za Dunia na kutambulika sokoni.
Pamoja na hatua hiyo, tutaendelea na kuboresha kosafu (sifa) za mifugo, kujenga Mabwawa ya kunyweshea, majosho, machinjio na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya ufugaji. Lengo ni kuwa na mnyororo wa kuongeza thamani ya mifugo na mazao ya mifugo, kwa ajili ya kuliendea soko la nje. Tutoke kwenye kumtazama ng’ombe na mlio wake, tutazame uzito wa nyama, ladha ya nyama, wingi wa maziwa, ubora wa ngozi, ubora wa kwato na pembe. Mtazamo huo ndio utakaoleta mapinduzi ya sekta ya mifugo.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye uvuvi, tunaenda kuongeza manufaa ya uvuvi wa Bahari Kuu na kwenye Maziwa Makuu. Tutakamilisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi iliyopo Kilwa, ambayo itazalisha fursa za ajira takriban elfu thelathini (30,000). Tutajenga bandari nyingine ya kisasa ya uvuvi kule Bagamoyo itakayofungamanishwa na kongani ya viwanda vya samaki. Tutafanya mapitio ya utoaji wa leseni za uvuvi kwa lengo la kuifanya nchi kufaidika ipasavyo na fursa za uvuvi wa bahari kuu.
Aidha, tutaendeleza utoaji wa mikopo ya boti, zana za uvuvi, makasha ya kuhifadhi samaki na miundombinu ya kukaushia. Vilevile, tutawekeza zaidi kwenye vizimba na mabwawa ya kufugia samaki, na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi. Hili litakwenda sambamba na kutafuta majawabu ya teknolojia ya chakula cha samaki ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwa wafugaji wa samaki (aquaculture).
Tutalipa kipaumbele suala la maendeleo ya uchumi wa buluu na sekta ya uvuvi, ikiwemo kilimo cha kisasa cha mazao ya baharini.
Mheshimiwa Spika;
Hatuwezi kufikia malengo yetu bila kuikuza sekta ya viwanda nchini. Hivyo, tumejiwekea lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya uzalishaji viwandani kutoka asilimia 4.8 hadi kufikia asilimia 9 kwa mwaka ifikapo 2030.
Katika kipindi kilichopita tuliweza kuanzisha kongani kubwa za viwanda na kuvutia wawekezaji wengi zaidi, ikiwemo kongani ya viwanda ya Kwala ambayo itakapokamilika itazalisha ajira za moja kwa moja laki moja (100,000) na zisizo za moja kwa moja laki tano (500,000), na pia Kongani ya Viwanda ya Buzwagi inayotarajia kuzalisha ajira laki tatu (300,000) itakapokamilika. Tutaongeza kongani nyingine mpya na ya kisasa kule Bagamoyo ambayo nayo inatarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wa Tanzania.
Tunapoanza safari ya muhula wa pili wa miaka mitano ya awamu ya sita, tunajipanga kuweka kongani za viwanda katika kila Wilaya ili tuongeze thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi, mifugo na madini tunayozalisha, na vitakavyoweza kuzalisha bidhaa zinazohitajika kwenye masoko ya maeneo yetu.
Tutahamasisha ujenzi wa viwanda vitakavyolisha viwanda vyengine, kwa malighafi na vipuri, na viwanda vitakavyozalisha bidhaa zinazohitajika kwenye masoko ya kikanda. Lengo la mkakati huu ni kuelekea kwenye Taifa linalojitegemea.
Mheshimiwa Spika;
Kuna viwanda ambavyo vimebinafsishwa lakini vimetelekezwa na havifanyi kazi. Hali hii, inakinzana na dhamira njema ya kuvibinafsisha, na pia inawakosesha wananchi soko na fursa za ajira. Kwa kuwa viwanda hivi vilikusudiwa kuongeza thamani ya mazao katika maeneo viliko, tutashirikisha vyama vya ushirika katika kuvifufua na kuviendesha. Lengo la Serikali ni kuona kuwa ushirika una uwezo wa kusambaza pembejeo, kuzalisha zaidi, kuendesha viwanda vya uongezaji thamani ya mazao, na kutafuta masoko pia.
Ili kuitekeleza vyema ajenda yetu ya uchumi wa viwanda, tutaendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ya umeme, maji, bandari, reli na barabara kwa ajili ya usafiri na usafirishaji wa malighafi na bidhaa. Tutafanya mapitio ya Sera na Sheria zetu za biashara ili kujenga mazingira wezeshi na bora ya kuvutia biashara na uwekezaji. Vilevile, tutaungana na majukwaa ya kimataifa ya uwekezaji barani Afrika na duniani kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuvutia wawekezaji wakubwa Duniani ili kufungua rasilimali zetu.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imebarikiwa sana na madini ya aina mbalimbali. Hadi sasa, eneo lililopimwa na kufanyiwa utafiti wa kina ni asilimia 16 tu ya eneo lote lenye miamba yenye madini nchini. Kazi yetu miaka inayokuja ni kuhakikisha madini haya yanawaletea maendeleo wananchi na kuwainua kiuchumi. Katika kipindi kilichopita, tuliweza kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024. Hatua hii inamaanisha madini yanachangia zaidi mapato kwa wananchi, makusanyo kwa Serikali, na uwekezaji kwenye huduma za kijamii.
Kuelekea mwaka 2030, tutakamilisha Mkakati wa madini adimu (critical minerals) ili Serikali itambue aina ya madini, viwango vya madini na eneo madini yalipo. Kwa kuwa Madini ya Kimkakati ndio yanayohitajika zaidi Duniani, tutaongeza umakini katika kusimamia uwekezaji wa madini hayo.
Katika jitihada zetu za kuendeleza sekta hii ya madini, tutapitia upya leseni zilizotolewa ili kubaini leseni ambazo hazijaendelezwa na kuchukua hatua za kuzitoa kwa wachimbaji wenye nia ya dhati ya kufanya uendelezaji wa maeneo husika. Wachimbaji wadogo wamekuwa nguzo ya kutegemewa katika sekta ya madini nchini. Hivyo basi, tutatenga maeneo maalum kwa ajili yao, tutawapatia leseni na tutawaendeleza kwa kuwapa mitaji na mitambo ya uchorongaji, pamoja na kuwapatia taarifa sahihi za kijiolojia.
Aidha, tutaendeleza utaratibu wa Benki Kuu kununua akiba ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati walio na leseni halali kutoka Tume ya Madini. Tunafanya hivi kuhakikisha wachimbaji wanapata mnunuzi wa uhakika, kupunguza utoroshaji wa madini na pia kurasimisha biashara ya uchimbaji kwa vijana wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kuimarisha masoko ya madini na vito. Kipekee kwa madini ya Tanzanite, tunaenda kumalizia jengo la Tanzanite Exchange Centre (TEC) katika eneo la Mirerani. Mbali na kuwa Nchi yetu ni mzalishaji mkubwa wa madini, tunataka ifikapo 2030 Tanzania iwe kituo kikuu cha uuzaji wa madini yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hatua nyingine muhimu katika kuongeza mchango wa Sekta ya madini katika maendeleo ya nchi ni kusimamia uongezaji wa thamani ya madini hayo hapahapa nchini.
Tunadhamiria kuwa na kiwanda cha kuchenjua madini (multipurpose refinery) ifikapo 2030. Tutaondokana na kusafirisha makinikia kwenda nje ili tuokoe ajira ambazo tumekuwa tukizipoteza. Vilevile, tutaanzisha Mfuko wa Wakfu wa Madini (Minerals Sovereign Wealth Fund) ili fedha zitokanazo na madini zije ziwafae vizazi vijavyo. Tunafanya hivyo tukitambua kuwa madini si mahindi kwamba ukiyavuna, utatenga mbegu ili uyaoteshe tena. Ukichimba madini kuna mwisho wake. Tunataka vizazi vyetu visikute mashimo tu, bali wakute fedha zitokanazo na madini tunayoyavuna leo.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imejaaliwa vivutio vingi vya utalii ambapo sekta hii ina mchango mkubwa sana kwenye uchumi.
Tunapoelekea 2030, tutaendelea kuikuza zaidi sekta hii tukilenga kufikia watalii wa ndani na nje milioni 8. Tunaamini kwamba, kutokana na wingi na ubora wa vivutio pamoja na utajiri mkubwa wa kitamaduni, tunaweza kufikia lengo hili. Sasa ili kukuza utalii tutafungamanisha vivutio vya utalii ili mtalii atumie siku nyingi zaidi akiwa hapa nchini. Vilevile, tutaboresha vyuo vyetu vya utalii na ukarimu, kwa kuongeza idadi ya watoa huduma wenye weledi katika fani zote kwenye hii sekta ya utalii na ukarimu. Sekta hii nayo ni sehemu muhimu ya mpango wa kuzalisha ajira zaidi kwa wananchi na kutuongezea akiba ya fedha za kigeni.
Tutaendeleza pia jitihada za uhifadhi na utunzaji wa maliasili sambamba na kupambana na ujangili. Aidha, hatuna budi kuongeza nguvu kukabiliana na changamoto ya wanyama waharibifu inayokabili jamii mbalimbali zinazopakana na hifadhi kote nchini. Niwaahidi kuwa Serikali itaongeza askari, vituo vya ulinzi, mbinu na vifaa vya kisasa ikiwemo ndege nyuki kukabiliana na athari hizi za wanyama waharibifu.
Mheshimiwa Spika;
Eneo lingine tutakalolipa uzito mkubwa ni sekta ya ujenzi. Kipaumbele chetu kitakuwa kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ambazo tayari zimeanza na zinaendelea. Tutaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara kupitia TANROADS, ili tufikie lengo letu la kuunganisha Wilaya zote na Makao Makuu ya Mikoa kwa kiwango cha lami.
Kwa jiji la Dar es Salaam, tutaboresha barabara kuu kwa kujenga barabara za juu katika makutano ya barabara katika maeneo ya Morocco, Mwenge, Magomeni na Tabata, na ujenzi wa awamu zilizobaki za miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT). Tutaijengea uwezo UDART ili iweze kusimamia vyema uendeshaji wa mabasi haya. Tutakamilisha pia ujenzi wa daraja muhimu, Daraja la Mto Msimbazi.
Tutaongeza pia bajeti na uwezo wa TARURA kuboresha barabara za ndani na za vijijini ili kuhakikisha zinapitika mwaka mzima, na kuwa wakulima wanaweza kuyafikia masoko kwa urahisi.
Kwa upande wa ujenzi wa makazi, jitihada zetu zitajielekeza kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ili tuwawezeshe wananchi kujenga makazi bora. Tutaweka mkazo maalum kwenye nyumba bora na nafuu. Tutasimamia utekelezaji wa sera zinazolenga kuboresha hali ya makazi kwenye maeneo yenye makazi duni. Tutashirikiana na sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji kwenye miradi ya uendelezaji miji kwa kujielekeza kwenye ujenzi wa nyumba za bei nafuu (yaani affordable housing).
Sambamba na hilo, tutaongeza kasi ya urasimishaji wa maeneo ya makazi, na kuimarisha utatuzi wa migogoro ya ardhi, kwa kupima ardhi nchi nzima kwa teknolojia ya kisasa ya satelaiti (Land Geo Spatial Technology).
Mheshimiwa Spika;
Hakuna maendeleo ya kiuchumi na kijamii bila nishati ya umeme wa uhakika na wenye nafuu. Hakuna. Katika kipindi kilichopita tuliweza kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kutoka Megawati 1,600 na kufikia Megawati 4,000 na pia tulifikisha miundombinu ya umeme kwenye kila kijiji. Tunapoelekea mwaka 2030, tumejiwekea lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme maradufu kufikia Megawati 8,000 na tutaendelea kupanua mtandao wa umeme ili kuvifikia vitongoji vyote nchini.
Tutaongeza uzalishaji kwa kutumia vyanzo vya nishati mbalimbali ambazo nchi yetu imebarikiwa nazo ikiwemo maji, jua, gesi, joto ardhi na upepo, na hata umeme utokanao na nguvu ya nyuklia. Vilevile, kupitia mpango wa Gridi Imara tutakamilisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme na tutaongeza vituo vya kupoza umeme ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi na makazi yanapata umeme wenye nguvu inayotakiwa. Lengo letu ifikapo 2030, mikoa yote ya Tanzania iwe imeunganishwa na gridi ya Taifa ya umeme.
Ili kuihakikishia nchi usalama wa nishati ya mafuta, tutaboresha miundombinu ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari zetu na maeneo ya kimkakati.
Tutasimamia utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia. Lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia Nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, hatua itakayopunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya za watumiaji.
Kwa upande wa gesi asilia, niwatoe hofu kuwa tupo kwenye hatua nzuri za majadiliano. Tuna dhamira ya dhati ni kukamilisha majadiliano hayo ya mradi huu mkubwa na wa kihistoria wa dola bilioni 42 wa uchimbaji wa gesi asilia. Kama tutakubaliana na wawekezaji, Mradi huo utabadilisha kabisa taswira na sura ya uchumi wetu. Katika majadiliano yetu tumechelewa kidogo kwa sababu tunahakikisha majadiliano hayo yanazingatia maslahi mapana ya nchi na kuhakikisha mradi huu utawanufaisha Watanzania moja kwa moja. Vilevile, tutajielekeza pia kwenye kuongeza utafiti wa gesi asilia maeneo ya baharini na nchi kavu.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kuwa Tanzania ni lango kuu la kuzifikia nchi nyingine za Afrika ya Mashariki na kusini mwa Afrika, tunalazimika kuwekeza sana kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ili tuweze kuwahudumia vyema ndugu zetu ambao hawakupata bahati ya kuwa na milango ya kuingia na kutoka kwa njia ya bahari. Hii ndiyo njia pekee ya kunufaika na fursa yetu ya kijiografia. Ni kwa msingi huo, tunaendeleza uwekezaji kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ya ushoroba wa kati kwa kukamilisha vipande vilivyosalia, yaani Makutupora-Tabora; Tabora-Isaka; Isaka-Mwanza; na Tabora-Kigoma, na vilevile, kipande kinachoenda Burundi cha Uvinza-Musongati. Tutakuja na mkakati wa kuhakikisha reli inatengeneza ushoroba wa uchumi, biashara na uwekezaji.
Tunajipanga pia kujenga reli ya SGR kutoka Tanga hadi Musoma, na kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay (Ruvuma) inayofika pia Mchuchuma na Liganga. Sambamba na ujenzi wa reli mpya, tutasimamia maboresho ya reli zilizopo ikiwemo reli ya TAZARA. Ninafurahi kuwaatarifu kuwa hivi karibuni kutafanyika hafla ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Ukarabati wa Reli ya TAZARA itakayofanyika nchini Zambia. Aidha, kwa reli ya zamani ya Meter Gauge (MGR) tutafanya ukarabati wa vipande vya Tabora – Kigoma; Kaliua – Mpanda; Tanga – Arusha; Ruvu – Mruazi; ili nayo itumike kuchochea uchumi. Miradi yote hii itazalisha fursa nyingi za ajira kwa Watanzania.
Katika kushirikisha sekta binafsi, tutasimamia ujio wa waendeshaji binafsi kwenye reli zinazojengwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC). Kwa kuanzia tutakuwa na mwendeshaji binafsi kwenye reli ya TAZARA, hatua hii itazidi kupunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara.
Vilevile, tunakusudia kujenga treni za mijini za kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma ili kuboresha usafiri kwenye majiji haya yanayokua kwa kasi kubwa sana. Kwa mfano, Dar es Salaam inatarajiwa kuwa na wakaazi milioni 10 ifikapo mwaka 2030, hivyo, kurahisisha njia za usafiri ni kurahisisha shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika;
Tukiangazia upande wa uchukuzi, mwelekeo wetu wa kisera ni kujenga Mfumo Fungamanishi, yaani Multimodal Transport System, ambao utahakikisha kuwa bandari, viwanja vyote vya ndege, na vituo vya reli vina muunganiko wa usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia mbalimbali.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya maboresho ya miundo mbinu na mifumo ya uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, gharama za uendeshaji wa bandari zimepungua ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 258 kwa mwaka zimeokolewa. Fedha hizo zinatumika kuongeza uwekezaji kwenye bandari hiyo ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika;
Kuelekea mwaka 2030, tutasimamia maboresho zaidi kwenye bandari zetu nchini. Tutaongeza gati 10 kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa ina Gati 12. Tutakamilisha kuunganisha reli ya SGR na bandari ili mizigo isafirishwe kwa reli hadi Bandari Kavu ya Kwala ambapo magari ya mizigo (malori) yatafanya kazi ya usafirishaji kuanzia hapo.
Vilevile, tutazidi kuboresha bandari zetu za bahari ya Hindi ikiwemo Tanga, ambayo tutaiunganisha kwa reli na Bandari ya Musoma kule Mara. Tutafanya upanuzi na maboresho kwenye bandari ya Mtwara ambayo nayo, tunakusudia kuiunganisha kwa reli na Bandari inayojengwa Mbambabay kule Nyasa, Ruvuma. Bandari mpya itakayojengwa Bagamoyo itaunganishwa na Bandari kavu ya Kwala.
Halikadhalika, tutaziendeleza bandari zetu za maziwa makuu za Mwanza, Kigoma, na Kalema kule Tanganyika na tutakamilisha ukarabati na ujenzi wa meli za abiria na mizigo zitakazotoa huduma kupitia bandari hizo, ikiwemo MV Mwanza ambayo imeshaanza kutoa huduma za usafirishaji kule Kanda ya Ziwa. Sambamba na hilo, tutakamilisha upatikanaji wa meli kubwa itakayotoa huduma katika Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa usafiri wa anga, pamoja na mambo mengine, tumepanga kuwa ifikapo mwaka 2030 tuliimarishe zaidi Shirika letu la Ndege la Tanzania kwa kuongeza ndege mpya 8 kuliwezesha shirika kuongeza miruko ndani na nje ya nchi. Mwelekeo wetu ni kufungua nchi pamoja na kukifanya kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kuwa kiungo (hub) cha safari za ndege kimataifa.
Aidha, tutakamilisha ujenzi wa viwanja mbalimbali unaoendelea, vikiwemo Kiwanja cha Kimataifa cha Msalato – Dodoma, na viwanja vya Mwanza, Iringa na Mpanda. Aidha, tutaongeza viwanja vikubwa hasa vilivyopo pembezoni mwa nchi kwa lengo la kuendelea kupanua biashara na utalii. Miongoni mwa miradi hiyo ni viwanja vya ndege vya Mugumu kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; Kiwanja cha Ndege cha Njombe kukuza biashara ya mazao na matunda na kurahisisha usafirishaji wake; na Kiwanja cha Ndege cha Kyabajwa, Kagera kitakachofungua fursa zaidi kwa mkoa wa Kagera.
Serikali itajenga Chuo Kikuu cha Anga cha Taifa na kuimarisha mafunzo na kuvutia zaidi wataalam wakiwemo marubani, wahandisi na wahudumu wa ndege.
Mheshimiwa Spika;
Tunapotekeleza Mkakati wa Uchumi wa kidijitali, uwekezaji kwenye TEHAMA ni muhimu sana. Hivyo, tutaendeleza kazi ya kuhakikisha mifumo yetu inasomana ikiwemo mifumo mipya inayoanzishwa. Tutaongeza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akili unde (artificial Intelligence) ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma.
Kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kampuni za watoa huduma, tutahakikisha huduma ya mtandao inawafikia Watanzania wengi zaidi ili iwasaidie kujiunga katika mifumo ya upatikanaji wa fedha na mitaji (Financial Inclusion) na kukuza biashara zao. Tutajenga pia Chuo cha Teknolojia ya Kidijitali (Digital Technology Institute) ili kuwajengea vijana wetu uwezo wa kushindana katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika;
Utunzaji wa Mazingira ni suala muhimu sana katika maendeleo tunayoyapanga na kuyatarajia. Kuelekea 2030, tutaimarisha usimamizi wa biashara ya hewa ukaa (Carbon Trade) kwa manufaa ya wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla. Vile vile hatua hii itasaidia kupunguza migogoro ya mikataba katika siku za usoni.
Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari ili Watanzania wapate haki yao ya kupata taarifa za ndani na nje ya nchi. Tutaendelea kutoa leseni kwa vyombo vya habari, na kulinda uhuru wa kufanya kazi zao, kwa kufuata sheria za nchi. Tutaimarisha vitengo vya habari vya Serikali ili viweze kutoa habari kwa weledi na kwa wakati. Aidha, tutaendelea kutambua waandishi wa habari za maendeleo nchini kupitia Tuzo ya Samia Kalamu Awards.
Mheshimiwa Spika;
Maendeleo ya nchi yoyote yanaonekana katika utamaduni na ustaarabu wake. Isitoshe katika dunia ya leo, utamaduni ni bidhaa na utamaduni ni uchumi. Hivyo, tutakuza na kuifanya lugha yetu ya Kiswahili kuwa bidhaa.
Vilevile, tunaendelea na maandalizi ya ujenzi wa studio ya kisasa ya filamu ili kupandisha thamani ya kazi za wacheza filamu wetu hapa nchini.
Tutajenga ukumbi wa kisasa wa maonyesho ili kuwawezesha wasanii wetu kufanya matamasha ya kimataifa, na kuvutia wasanii wa nje wakubwa kufanya matamasha nchini.
Tunataka sanaa, filamu na muziki zitengeneze ajira na kuchangia uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Spika;
Michezo ni uchumi. Hatuwezi kupata matokeo makubwa bila kuwekeza. Miongoni mwa hatua tutakazozichukua ni kuanzisha na kuendeleza shule za michezo (sports academies) kwa lengo la kuwaandaa wanamichezo wa leo na kesho.
Kama mnavyofahamu, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON mwaka 2027, na kuelekea huko tutakamilisha ujenzi wa viwanja vitakavyotumika, ikiwemo Uwanja wa AFCON uliopo Arusha, na maboresho ya viwanja vingine nchini. Vilevile, tutaendelea kuvutia michezo mbalimbali kufanyika hapa nchini ili kuongeza fursa zitokanazo na kuwa mwenyeji wa michezo hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania inathamini ushirikiano wa kimataifa na ingependa kuishi na mataifa mengine kwa misingi ya kuheshimiana na kufaana. Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo na nchi marafiki na mashirika ya kimataifa. Daima tutajielekeza katika kuongeza marafiki, na kupanua fursa za kiuchumi kwa nchi yetu na watu wake.
Kama Taifa, tunapenda tuheshimiwe kama sisi tunavyoheshimu mataifa mengine. Na katika kulinda maslahi ya Nchi, hakuna mbadala. Ni lazima tuhakikishe tunalinda utu, heshima na uhuru wetu. Tutaendelea kuongozwa na misingi ile ile ya Sera ya Nje iliyoasisiwa na waasisi wa nchi yetu ya kutofungamana na upande wowote. Msimamo wetu ni umoja na ushirikiano badala ya mgawanyiko, majadiliano badala ya amri/mabavu, na haki badala ya visasi. Taifa la Tanzania limejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa; nguvu yoyote inayokusudia kuchafua misingi hiyo hatutokubaliani nayo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande mwingine, tutaendelea kuviimarisha vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama ili tuhakikishe ulinzi wa mipaka yetu, na ulinzi wa raia na mali zao. Vilevile, Taifa la Tanzania litaendelea pia kutimiza wajibu wake wa kuchangia misheni za ulinzi wa amani za kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Spika;
Tumezungumzia masuala mengi, ila msingi wa mafanikio yote haya ni utawala wa sheria, uadilifu na uwajibikaji katika kila ngazi, kuanzia juu mpaka chini. Kwa msingi huo, na ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za nchi pamoja na kupata huduma wanazostahili, tutaelekeza jitihada zetu kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uzembe, ukosefu wa nidhamu na ukosefu maadili. Ni lazima tudhibiti wachache wanaotaka kuturudisha nyuma kwa kuendekeza maslahi binafsi.
Aidha, ili kuimarisha uwajibikaji Serikalini, tutaendelea kutekeleza programu za maboresho ya utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya upimaji wa utendaji kazi. Wajibu huenda na haki, au haki huambatana na wajibu. Hivyo basi, pamoja na kuwataka watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo, tutaendelea kuboresha maslahi yao kadri uchumi utakavyoruhusu.
Mheshimiwa Spika;
Vile vile, tutaimarisha uwajibikaji na utendaji wa mashirika ya umma. Kuelekea 2030, tutafanya mageuzi ya mashirika ya umma ili kuboresha ufanisi, uwazi na tija. Tunataka kuongeza sio tu gawio ambalo Serikali inapokea, lakini pia kufikia lengo la Mashirika na Taasisi za Umma kuchangia angalau asilimia 10 ya mapato yote yasiyo ya kodi.
Nia yetu ni kuyajengea uwezo Mashirika ya Umma yaweze kushindana na kuwekeza nje ya Tanzania, kama mashirika mengine ya nje tunavyoyaona hapa nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika;
Msingi mwingine wa mafanikio yote haya ni utawala wa sheria. Ahadi yetu ni kuwa Serikali itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wote na kwa wakati. Tutaendelea kuwezesha Mahakama kwa majengo, vitendea kazi, watumishi pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA. Tunachukua hatua zote hizi ili Mhimili huu uweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Tutasimamia utekelezaji kamili wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya kuangalia namna ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Tutaendelea kufanya mageuzi na maboresho katika taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu.
Kwa upande mwingine, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya Sheria, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) pamoja na asasi zingine ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi, kwani katika kipindi kilichopita tumeona manufaa yake katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Aidha, tutakamilisha tafsiri ya sheria zetu zote kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu kuhakikisha wananchi wetu wanaelewa kwa urahisi sheria za nchi.
HITIMISHO NA KUFUNGUA BUNGE LA 13
Mheshimiwa Spika;
Sikuweza kuyasema yote yatakayofanyika ndani ya miaka mitano ijayo kwa kuwa muda hauruhusu. Bila shaka, nitapata wasaa mwingine wa kulihutubia Bunge hili tukufu siku zijazo. Katika shughuli za kawaida za bunge, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu mawaziri nitakaowateua hivi karibuni, chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, watapata wasaa wa kufafanua kwa kina maeneo niliyoyagusia pamoja na maono ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo. Aidha, ikikupendeza, Mheshimiwa Spika, hotuba hii ikajadiliwa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali itakuwa tayari kupokea maoni, ushauri na mapendekezo yenu kwa moyo mkujunfu ili tuweze kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika;
Naliahidi Bunge lako Tukufu ushirikiano wangu binafsi na wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuyatekeleza yote haya kwa manufaa ya Watanzania ambao Wabunge hawa wanawawakilisha. Rai yangu kwenu ni kutoa ushirikiano wa dhati kwa Serikali. Kwa pamoja, tutajenga Nchi ambayo mifumo inafanya kazi na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi ili Watanzania nao waweze kufanya kazi zao kwa bidii na weledi kwa maendeleo ya Taifa letu. Namuomba Mwenyezi Mungu kuwa mwisho wa utumishi wa Awamu ya Sita usipimwe tu kwa vitu vitakavyoachwa, bali pia kwa tabasamu la utu litakaloachwa kwenye nyuso za Watanzania.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kusema hayo, sasa ninayo heshima ya kutamka kwamba Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa limefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Ahsanteni kwa kunisikiliza


