Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limesema mpango wa Marekani kuwapeleka wahamiaji katika nchi za Afrika unakiuka sheria ya haki ya kimataifa, na lazima ukataliwe.
Katika siku za hivi karibuni, Eswatini, Ghana, Rwanda na Sudan Kusini zimewapokea wahamiaji kutoka Marekani, kama sehemu ya mpango wa utawala wa Rais Donald Trump kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali, chini ya ”mikataba isiyoeleweka”.
Shirika hilo limesema mkataba kati ya Marekani na Eswatini, ambao bado haujawekwa wazi, ulihusisha dola milioni 5.1 kwa ajili ya kujenga uwezo wake wa usimamizi wa mipaka na uhamiaji.
Kwa upande wake, Eswatini ilikubali kuwapokea hadi wahamiaji 160 waliofukuzwa Marekani.
Kulingana na shirika hilo, Rwanda ambayo imeripotiwa kukubali kuwapokea hadi wahamiaji 250 waliofukuzwa Marekani, itapatiwa msaada wa kifedha wa takribani dola milioni 7.5.
Mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Afrika, Allan Ngari amesema makubaliano hayo yanazifanya nchi za Afrika kuwa washirika wa utawala wa Trump unaokiuka haki za binaadamu za wahamiaji.
Shirika hilo limezitaka serikali za Afrika kukataa kuwakubali wahamiaji kutoka Marekani na kuvunja mikataba ambayo tayari inatekelezwa.
Ngari amesema nchi hizo zinapaswa kuhakikisha hakuna mtu anayerejeshwa katika nchi yake ikiwa kuna ushahidi kwamba anaweza kudhuriwa.
