Mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 nchini Indonesia. Haya yamesemwa leo na maafisa wa uokoaji nchini humo.
Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Maafa limesema maafa hayo, ambayo yamekumba kisiwa cha kaskazini-magharibi cha Sumatra katika muda wa wiki mbili zilizopita, yamesababisha vifo vya watu 1003, 218 hawajulikani walipo na wengine zaidi ya 5,400 wamejeruhiwa.
Baada ya kuzuru eneo la Langkat katika mkoa wa Kaskazini wa Sumatra hii leo, Rais wa nchi hiyo Prabowo Subianto amesema hali imeimarika na maeneo kadhaa ambayo yalikuwa yamekatwa na mafuriko na maporomoko hayo sasa yanafikika.
Gharama za ujenzi mpya baada ya maafa hayo zinaweza kufikia dola bilioni 3.1 na hadi kufikia sasa, serikali ya Indonesia imepuuza mapendekezo ya kuomba msaada wa kimataifa.

