Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), mimea ni asilimia 80 ya chakula cha binadamu na asilimia 98 ya oksijeni. Pamoja na umuhimu huo bado iko kwenye tishio dhidi ya mazingira na viumbe wakiwemo wadudu, wanyama na shughuli za binadamu.
Kila mwaka, zaidi ya makontena milioni 240 husafirishwa kati ya nchi na nchi, yakiwa na bidhaa za mimea, na kuongeza hatari ya usalama wa mimea na viumbe hai. Kwa mantiki hiyo ulinzi wa mimea umekuwa ni jambo linalopewa kipaumbele na dunia, kwa sababu ya umuhimu wake kwa uhai wa binadamu.

Kila tarehe Mei 12, dunia huadhimisha Siku ya Afya ya Mimea iliyoanzishwa ili kuhamasisha umuhimu wa kulinda afya ya mimea kwa ajili ya uzalishaji endelevu wa chakula, ulinzi wa mazingira na uchumi wa dunia.
Tunakuletea mimea mitano kati ya mimea kadhaa inayolindwa kwa kiwango cha juu duniani. Mimea hii si tu adimu, bali pia ina umuhimu mkubwa wa ikolojia, kihistoria na hata kitamaduni. Mataifa na mashirika kadhaa dunia hutumia mabilioni ya fedha kuhakikisha afya na uhai wa mimea hii. Na watetezi wa mimea wanatoa wito wa kulindwa kwa mimea hii kama yanavyolindwa madini ya almasi.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) na mashirika mbalimbali ya mazingira, mimea hii iko katika hatari ya kutoweka, na hivyo kuhitaji hatua za haraka za uhifadhi na kuilinda.
1. Welwitschia mirabilis

Welwitschia ni mmea wa kipekee unaopatikana katika jangwa la Namib, kusini mwa Angola na Namibia. Ingawa ina majani mawili tu, huweza kuishi kwa zaidi ya miaka 1,000. Kwa mujibu wa Botanical Society of Namibia, mimea hii huchukua maji kutoka kwenye ukungu wa asubuhi na hivyo kustahimili mazingira yenye unyevunyevu mdogo.
Utafiti uliochapishwa na Kew Gardens, Uingereza, unaeleza kuwa mfumo wa ukuaji wa Welwitschia ni wa kipekee na haupatikani katika spishi nyingine za mimea duniani.
Kwa sababu ya hali ya hewa inayoendelea kubadilika, shughuli za uchimbaji madini na utalii holela, Welwitschia sasa inalindwa chini ya sheria za mazingira za Namibia. Serikali ya Namibia, kwa kushirikiana na taasisi kama UNESCO, imeweka maeneo ya uhifadhi ambapo mimea hii inalindwa, ikiwemo Skeleton Coast National Park. Hii ni mojawapo ya mimea inayotazamwa kama alama ya urithi wa asili wa dunia.
2. Dragon’s Blood Tree

Mti huu unaopatikana katika kisiwa cha Socotra nchini Yemen, hujulikana kwa jina la kisayansi Dracaena cinnabari. Muonekano wake wa kipekee kama mwavuli unaofunguka juu, pamoja na utokaji wa utomvu mwekundu kama damu, umekuwa ukivutia watafiti kwa karne nyingi.
Kwa mujibu wa World Wildlife Fund (WWF), mti huu ni kiashiria cha urithi wa kipekee wa visiwa vya Socotra ambavyo vina zaidi ya 700 ya spishi adimu zisizopatikana kwingine duniani.
Shughuli za ufugaji usio endelevu, ukataji miti na mabadiliko ya tabianchi vinaweka spishi hii katika hatari. Shirika la UNESCO limeitaja Socotra kama moja ya sehemu za urithi wa dunia na juhudi za uhifadhi zinafanywa kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa.
Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na IUCN (2023), mti huu unaorodheshwa kama mti ulio hatua moja kabla ya kuingia kwenye kundi la mimea iliyoko hatarini kutoweka.
3. Rafflesia arnoldii

Rafflesia ni ua lenye kipenyo kinachoweza kufikia sentimita 100, na linaweza kufika hadi kilo 10. Hupatikana katika misitu yyenye mvua nyingi ya Asia ya Kusini Mashariki, hasa Indonesia, Malaysia na Ufilipino.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Smithsonian, ua hili halina mizizi wala majani yake yenyewe bali hutegemea kikamilifu mimea mingine kama mwenyeji wake. Harufu yake kali kama nyama iliyooza huvutia nzi ambao husababisha uchavushaji.
Hata hivyo, uharibifu wa misitu kwa ajili ya kilimo, ukataji miti na ujenzi umefanya spishi nyingi za Rafflesia kuwa hatarini. Utafiti wa Global Environment Facility (GEF) unaonyesha kuwa zaidi ya spishi 18 za Rafflesia zinakabiliwa na hatari ya kutoweka, na nyingi hazijaorodheshwa rasmi kutokana na uhaba wa takwimu. Serikali ya Indonesia imeanzisha hifadhi maalum za bioanuwai kusaidia kulinda mimea hii na mfumo wa ikolojia unaoiunga mkono. Mamilioni ya fedha yanatumika kwa ajili ya hilo.
4. Orchids Pori

Orchids ni familia kubwa zaidi ya mimea ya maua duniani, zikiwa na zaidi ya spishi 25,000. Lakini spishi za porini, hasa zile zinazopatikana maeneo ya milima ya Afrika Mashariki kama Usambara, Uluguru na Mau (Kenya), zinakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka.
Kwa mujibu wa Convention on International Trade in Endangered Species (CITES), aina nyingi za orchids ziko katika orodha ya mimea inayohitaji uangalizi maalum kutokana na biashara haramu ya maua na uharibifu wa makazi yao asilia.
Orchids pori hupatikana kwa nadra sana na hukua kwa muda mrefu wakati mwingine huchukua miaka 5 hadi 10 kuchanua kwa mara ya kwanza. Kwa sababu hiyo, taasisi za misitu kama ya Tanzania Forest Services (TFS) na WWF Tanzania zimeanza miradi ya uhifadhi na uhamasishaji kwa jamii zinazozunguka maeneo ya milima ili kusaidia katika upandaji wa orchids na kuzuia uvunaji haramu.
5. Baobab (Adansonia)

Baobab ni mti maarufu barani Afrika unaojulikana kwa uwezo wake wa kuhifadhi maji ndani ya shina, kuishi kwa zaidi ya miaka 2,000, na kutoa matunda yenye virutubisho vingi. Huko Madagascar, baadhi ya spishi sita kati ya tisa za Adansonia zimeorodheshwa na IUCN kama “zilizo hatarini” kutokana na uharibifu wa misitu na ongezeko la matumizi ya ardhi kwa kilimo. Hata nchini Tanzania, mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika maeneo kame yameanza kutishia baadhi ya maeneo yaliyo na baobab.
Kwa mujibu wa FAO, baobab ni muhimu si tu kwa mazingira, bali pia kwa usalama wa chakula na uchumi wa jamii za vijijini. Hifadhi za asili kama ya Kilombero na maeneo ya Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) zimekuwa zikijumuisha uhifadhi wa miti ya baobab kama sehemu ya urithi wa kimazingira. Serikali na taasisi za kijamii zimekuwa mstari wa mbele kuelimisha kuhusu thamani ya mti huu na kupiga marufuku ukataji holela katika baadhi ya maeneo.
Makaya haya kwa msaada wa mtandao BBC Swahili