Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Mwalimu, amekisifu na kukipongeza chama chake kwa kuja na vipaumbele tisa vinavyogusa maisha ya wananchi na huku akiamini serikali ijayo itafanyia kazi vipaumbele hivyo na hatimaye kufanikisha azma ya serikali ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na kukuza ustawi wao.

Ummy ameyasema hayo Mei 30, 2025, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Ilani ya CCM ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kuwasilisha vipaumbele hivyo mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM waliokutana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akielezea furaha yake kuhusiana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, Ummy amesema “Mambo yote ya kwenye Ilani ni mazuri, na Ilani ya mwaka huu haina mambo mengi sana, ni mambo tisa muhimu yanayogusa maisha ya wananchi ya kila siku ya Mtanzania.

Ukiangalia masuala ya miundombinu ya uchumi, huduma za afya, lakini kubwa nimevutiwa kuona vipaumbele vikihusisha suala la kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, hiki kimekuwa kilio cha vijana wa Kitanzania hususani wanaomaliza vyuo vikuu”.

Sambamba na hilo, Ummy amesema kwa kuwa yeye ni mwanachama wa CCM anawajibika kukitekea chama chake kwa nguvu na wivu mkubwa, hivyo atashiriki kikamilifu kuinadi Ilani ya CCM ili kuhakikisha ushindi unapatikana. “Tuko tayari kwenda kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na kutafuta ushindi wa Chama Cha Mapinduzi katika nafasi ya Rais, Mbunge na Madiwani,” amesisitiza Ummy.

Ikumbukwe kuwa CCM imezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi 2025-2030 huku ikibeba vipaumbele tisa muhimu ambavyo zitanadiwa nchi nzima ili kuomba ridhaa ya wananchi kuelekea miaka ijayo 2025-2030. Vipaumbele hivyo ni kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa, kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuongeza kipato kwa watu, kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii.

Vipaumbele vingine ni kuongeza kasi ya maendeleo vijijini, kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kukuza na kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Vilevile, kudumisha amani, utulivu na usalama wa nchi yetu, kudumisha demokrasia na utawala bora na kudumisha utamaduni wa Taifa na kukuza sanaa ya nchi yetu.

Tayari vikao halali vya CCM kwa kauli moja vimewapitisha Dk. Samia Suluhu Hassan kupeperusha bendera ya Uras wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiwa mgombea mwenza wake. Kwa upande wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi ndiye mgombea wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025.