Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima, akizungumza katika mafunzo ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki (BVR) wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Mei 15, 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, litakalofanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu), Dkt. Rose Likangaga na kulia ni Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kilosa na Mikumi, Betuely Ruhega. Picha na INEC.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima, amesema Tume haitamvumilia mtu yeyote atakayehusika na kuvuruga zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kujiandikisha katika vituo zaidi ya kimoja.

Kailima ametoa onyo hilo Mei 15, 2025, wakati akizungumza katika mafunzo ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki (BVR) wa Wilaya za Kilosa na Mvomero, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa uboreshaji wa daftari hilo, litakalofanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, mwaka huu.

Amesema Serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio hivyo Tume haitomvumilia mtu yeyote atakayejaribu kufanya udanganyifu kwa lengo la kutia doa zoezi hilo.

Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima, akizungumza katika mafunzo ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki (BVR) wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Mei 15, 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, litakalofanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025. Picha na INEC

Aidha, Kailima amewataka waandishi wasaidizi na waendesha vifaa hivyo vya BVR katika Halmashauri zote ambazo zoezi hilo litakapoanza Mei 16 hadi 22, 2025, kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na utunzaji wa vifaa vya kazi vitakavyotumika katika zoezi hilo.

“Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa weledi na uzalendo, ili kuhakikisha hakuna dosari yoyote inayoibuka,” alisema Kailima

“Tumeweka jitihada kubwa kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa, jukumu la utunzaji wa vifaa ni la kila mmoja wenu, tuonyeshe uwajibikaji wa hali ya juu,” alisisitiza Kailima.

Katika hatua nyingine Kailima ameupongeza Mkoa wa Morogoro kwa kufanya vizuri katika awamu iliyopita ya uandikishaji, ambapo watu 147,000 waliandikishwa idadi hiyo ni sawa na asilimia 10 ya jumla ya watu zaidi ya milioni 1.3 walioandikishwa nchini.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima (aliyevaa kofia), akimwangalia mwendesha vifaa vya Bayometriki (BVR) alipokuwa anatoa huduma wakati wa mafunzo ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Mei 15, 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, litakalofanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025. Picha na INEC.

Sambamba na hayo amewataka wananchi kuacha tabia ya kuchana au kuharibu karatasi za orodha ya wapiga kura zilizobandikwa kwenye vituo vya kujiandikishia kwani kitendo hicho kinaweza kuzuia watu wengine kuhakiki taarifa zao, jambo ambalo linaweza kuwanyima haki yao ya kupiga kura iwapo taarifa zitakuwa na hitilafu.

Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kilosa na Mikumi, Betuely Ruhega ameishukuru Tume kwa kurahisisha mchakato wa uandikishaji, ambapo sasa mtu anaweza kujiandikisha au kubadilisha taarifa zake kwa njia ya mtandao, kisha kwenda kituoni kuchukua kitambulisho chake bila kupoteza muda jambo ambalo limetoa fursa kwa watu kuweza kujiandisha na kuahakiki taarifa zao.

Ameongeza kuwa mfumo huo ni rafiki kwa watu wote, wakiwemo wenye ulemavu, kwani waandishi wasaidizi na waendesha vifaa BVR wamepewa maelekezo ya kuzingatia hali ya kila mtu wakati wa kuchukua alama za vidole, picha na saini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu), Dkt. Rose Likangaga akitoa elimu ya Mpiga Kura katika mafunzo ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki (BVR), Wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro, Mei 15, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, litakalofanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025. Picha na INEC.

Uboreshaji wa daftari hili unalenga kuwapa nafasi wapiga kura wapya kujiandikisha, pamoja na kuwahakikishia wapiga kura waliopo kuwa taarifa zao ni sahihi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili litaingia katika mzunguko wa pili kuanzia Mei 16 hadi Mei 22, 2025, likihusisha mikoa ya Pwani, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Manyara, Lindi, Mtwara, Morogoro na Dar es Salaam kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na Mikoa yote ya Tanzania Zanzibar.

Baadhi ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki (BVR) wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Ramadhani Kailima (hayupo pichani), wakati alipokuwa akizungumza katika mafunzo ya waandishi na waendesha vifaa vya Bayometriki, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Mei 15, 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, litakalofanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025. Picha na INEC.