Na Dotto Kwilasa,JamhuriMediaDodoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo Julai 26, 2025 imezindua rasmi Kalenda ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa INEC jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa uchaguzi wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini, wanahabari na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji (Rufaa) Jacobs C. M. Mwambegele amesema kalenda hiyo ni nyenzo ya uwazi, uwajibikaji na ushirikiano wa kitaifa, inayotoa mwelekeo wa maandalizi ya uchaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 41(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024.
Amesema utoaji wa fomu kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais utafanyika kuanzia Agosti 9 hadi 27, 2025 huku Wagombea wa Ubunge na Udiwani watachukua fomu kuanzia Agosti 14 hadi 27, 2025 ambapo Uteuzi rasmi wa wagombea wote utafanyika tarehe 27 Agosti, 2025.
Amefafanua kuwa Kampeni za uchaguzi zitaanza mara baada ya uteuzi, kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 kwa upande wa Tanzania Bara, na Zanzibar kampeni zitafungwa Oktoba 27, 2025 ili kupisha upigaji wa kura ya mapema.

Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele ametangaza kuwa jumla ya wapiga kura 37,655,559 wameandikishwa kwa mwaka huu, ongezeko la asilimia 26.55 kutoka uchaguzi wa mwaka 2020. Kati ya hao, wanawake ni 18,943,455 sawa na asilimia 50.31, huku wanaume wakiwa 18,712,104 sawa na asilimia 49.69.
Aidha Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura umefanyika kwa awamu mbili kati ya Julai 2024 hadi Julai 2025.
Amefafanua kuwa Wapiga kura wapya waliosajiliwa ni 7,641,592, huku 4,291,699 wakiboresha taarifa zao.
Licha ya hayo amesema watu 99,744 wameondolewa kwenye daftari kwa kupoteza sifa, na 8,703 waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja taarifa zao zimekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.

Amezungumzia pia kwa upande wa Zanzibar, kuwa jumla ya lwapiga kura 725,876 walioandikishwa na ZEC watahusika katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge wa majimbo ya Zanzibar, huku wengine 278,751 waliokosa sifa za kuandikishwa ZEC wakiorodheshwa na NEC.
Jaji Mwambegele amesema jumla ya vituo vya kupigia kura 99,911 vitatumika katika uchaguzi huu, vikiwemo 97,349 kwa Tanzania Bara na 2,562 kwa Zanzibar. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 22.49 kutoka vituo 81,567 vilivyotumika mwaka 2020.
Aidha, INEC imezitaka taasisi za habari kuzingatia maadili na kutoa taarifa sahihi bila upendeleo wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
Pia imewataka viongozi wa dini na wazazi kutoa elimu ya uraia kwa vijana na jamii kwa ujumla.

Pamoja na hayo amesemeahidi kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa uchaguzi ili kuhakikisha amani, uwazi na ufanisi katika mchakato mzima, huku ikiahidi kutoa miongozo ya kisheria, ratiba ya kampeni na maadili ya uchaguzi mapema kwa utekelezaji wa majukumu ya wadau wote.
“Kura yako ni haki yako, jitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu,” amesema Jaji Mwambegele.
Uchaguzi wa mwaka 2025 unatarajiwa kuwa wa kwanza kufanyika chini ya sheria mpya ya uchaguzi, na unatarajiwa kutumia teknolojia zaidi katika usimamizi na uwasilishaji wa matokeo.
