Saa kadhaa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuitaka Iran “isalimu amri” ili kusitisha vita vinavyoendelea, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ameapa kuwa kamwe taifa lake halitajisalimisha kwa Marekani na Israel.
Ameyasema hayo kupitia hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa mapema Jumamosi. Katika hotuba hiyo Pezeshkian ameyaomba radhi mataifa jirani kwa mashambulizi yaliyofanywa na Iran.
Amesisitiza kuwa uongozi wa mpito wa nchi yake umemekubaliana kuwa hakutakuwa tena na mashambulizi ya aina hiyo dhidi ya maeneo ya nchi hizo isipokuwa pale Iran itakaposhambuliwa kutoka kwenye mataifa hayo.
Israel na Marekani, zilianzisha mashambulizi yaliyomuuwa Kiongozi wa juu zaidi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei Februari 28 hali iliyochochea mzozo wa kikanda. Tangu wakati huo, Iran ilijibu kwa kurusha makombora na droni katika vituo na miundombinu ya Israel na Marekani katika nchi za Mashariki ya Kati hasa eneo la Ghuba.


