IRAN na Marekani zinatofautiana kuhusu njia na mikakati ya kuiondolea Tehran vikwazo ili Iran iachane na kile Marekani inachosema ni nia yake yakudhibiti silaha za nyuklia.
Afisa mmoja wa Iran aliyezungumza na shirika la habari la Reuters amesema mazungumzo mapya kati ya pande hizo mbili yamepangiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Machi.
Afisa huyo alisema Tehran inaweza kuridhia kusafirisha sehemu ya madini yake ya Urani ambayo yamesharutubishwa pamoja na kupunguza nguvu ya madini hayo lakini lazima kwanza haki ya Iran ya kurutubisha madini hayo kwaajili ya shughuli za amani itambuliwe.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araqchi alisema siku ya Ijumaa kwamba, anatarajia kupata rasimu ya makubaliano ndani ya siku kadhaa kufuatia mazungumzo ya nyuklia yaliyofanyika kati ya Jamhuri hiyo ya kiislamu na Marekani.
Kulingana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Iran inamiliki zaidi ya kilo 400 ya urani ikiwa na urutubishwaji wa asilimia 60 ambayo inaweza kutumika katika utengenezaji wa silaha za nyuklia, iwapo urutubishaji huo utaongezeka na kufikia asilimia 90.


