Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amezipongeza juhudi za Pakistan za usuluhishi kati ya nchi yake, Marekani na Israel. Licha ya pongezi hizo, amesema uaminifu unahitajika ili kuutatua mzozo huo.

Ameyasema hayo katika mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya simu Jumamosi na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif. Aidha, Sharif amemweleza Rais Pezeshkian kuhusu mawasiliano ya kidiplomasia kati ya nchi yake na Marekani na mataifa mengine ya Ghuba.

Aidha Pezeshkian amezionya nchi za Ghuba ziache kutumiwa na Marekani kulishambulia taifa lake kama zinataka amani na usalama. Wawili hao wamezungumza wakati Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Saudi Arabia, Misri na Uturuki wakijiandaa kukutana Jumapili na Jumatatu katika juhudi za kuutatua mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati. Juhudi hizo zinafanyika wakati mashambulizi yakiendelea kushuhudiwa kote Mashariki ya Kati.