Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametangaza kuwa baraza jipya la uongozi limeanza rasmi kazi kufuatia kuuawa kwa Kiongozi Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, katika mashambulizi ya Marekani na Israel.
Katika ujumbe uliorekodiwa na kurushwa kwenye televisheni ya taifa, Pezeshkian amesema baraza hilo linajumuisha mkuu wa mahakama, Gholam Hossein Mohseni Ejehei, pamoja na mwanazuoni wa kidini Ayatollah Ali Reza Arafi, na litaiongoza nchi hadi kiongozi mpya atakapochaguliwa.
Wakati huo huo, milipuko imeripotiwa mjini Tehran huku Israel ikitangaza itaendelea na mashambulizi “yasiyokoma” dhidi ya viongozi na malengo ya kijeshi ya Iran. Iran nayo imerusha makombora kuelekea Israel na baadhi ya nchi za Ghuba kwa kulipiza kisasi.
Rais wa zamani wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ameripotiwa kuuawa katika shambulizi la anga mjini Tehran pamoja na mlinzi wake. Aliiongoza Iran kuanzia 2005 hadi 2013, lakini sera zake za nyuklia na matamshi yake yenye utata vilisababisha vikwazo vya kimataifa na kuifanya nchi hiyo kutengwa zaidi.
Serikali ya Iran imetangaza siku 40 za maombolezo ya kitaifa, huku mvutano ukizidi kuongezeka katika Mashariki ya Kati.


