Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amekataa mazungumzo ya ana kwa ana na Marekani kuujadili mpango wa nyuklia wa Iran.
Hatua hiyo huenda ikaondoa matumaini ya mwisho ya kuzuia kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.
Matamshi ya Khamenei, yaliyorushwa katika televisheni ya taifa ya Iran, yanaondoa uwezekano wowote wa Rais wa Iran Masoud Pezeshkian kukutana na maafisa wa Marekani.
Pezeshkian yuko mjini New York kuhudhuria Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.
Khamenei amesema hawahitaji silaha za nyuklia, na hawana mpango wa kutengeneza hata moja.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amekutana na mawaziri wenzake wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, kuhusu kurejeshwa kwa vikwazo, vinavyotarajiwa kuanza kutumika Jumapili.
Nchi hizo tatu pamoja na Umoja wa Ulaya, zimeitaka Iran kuchukua hatua ndani ya siku hizo kushughulikia wasiwasi juu ya mpango wake wa nyuklia.
