Mataifa ya Ufaransa, Ujerumani na Uingereza yamelaani vikali kile walichokiita vitisho vya Iran dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nishati ya Nyuklia (IAEA), Rafael Grossi.

Hatahivyo,Tehran imetupilia mbali lawama hizo, ikisema inahofia usalama wa wakaguzi wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, hasa baada ya mashambulizi ya kijeshi yaliyodaiwa kufanywa na Israel na Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia nchini humo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo tarehe 30 Juni 2025, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alisema haiwezekani kwa Iran kuendeleza ushirikiano wa kawaida na IAEA wakati ambapo usalama wa maofisa wa shirika hilo haujafafanuliwa wala kuhakikishwa.

“Tuna shaka kubwa kama usalama wa wakaguzi utaweza kulindwa katika mazingira haya ya mashambulizi. Si sahihi kutarajia ushirikiano wa kawaida,” alisema Baghaei.

Kauli hiyo imekuja baada ya Iran kukataa ombi la Grossi kutembelea vituo vya nyuklia vilivyohusishwa na mashambulizi ya hivi karibuni yanayodaiwa kufanywa na Israel na Marekani.

Iran imekanusha madai kuwa inamtishia Grossi, lakini imemkosoa kwa kile ilichodai ni taarifa zenye upotoshaji alizotoa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. SOMA: 

Grossi alinukuliwa akisema Iran imefikia karibu kiwango cha kutosha cha madini ya urani yaliyorutubishwa, ingawa haina nia ya kuunda silaha za nyuklia.

Iran na mataifa ya Magharibi yamekuwa katika mvutano wa muda mrefu kuhusu mpango wake wa nyuklia, huku mataifa ya Ulaya yakionya kuwa hatua za Iran ni tishio kwa usalama wa kimataifa na uthabiti wa mashirika ya kimataifa kama IAEA.