Israel imefanya wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran siku ya Jumapili wakati Tehran nayo ikijibu kwa makombora mapya. Pande zote mbili zimetishia kufanya uharibifu zaidi katika mzozo ambao unaonekana kufukuta zaidi.

Mamlaka za Israel zimewaelekeza raia kuelekea kwenye maeneo salama ya kujikinga na mashambulizi, wakati Iran ikisema kuwa itaanza kufungua misikiti, vituo vya treni za metro na shule ili kutumika kama maeneo ya kujihifadhi, wakati Israel ikiendeleza mashambulizi. Vyombo vya habari vya Iran vyaripoti mlipuko mjini Tehran

Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa Mkuu wa ujasusi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi Mohammed Kazemi, ni miongoni mwa majenerali watatu waliuawa katika mashambuliziya Israel jana Jumapili.

Wizara ya afya ya Iran imeripotivifo vya watu 224 tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo mapema siku ya Ijumaa. Watu wengine zaidi ya 1,200 wamejeruhiwa, asilimia kubwa wakiwa ni raia.

Kwa upande wa Israel, mamlaka zimeripoti vifo vya watu 13 tangu Iran ilipochukua hatua ya kujibu mashambulizi.

Israel inasema mashambulizi yake yamepiga vituo vya kijeshi na nyuklia, na kuua maafisa wakuu na wanasayansi wa atomiki, lakini afisa mkuu wa Marekani alisema Jumapili kwamba Rais Donald Trump aliiambia Israel iachane na mpango wa kumuua kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei.

Wakati huo huo, maeneo ya makazi katika nchi zote mbili yameshambuliwa pakubwa tangu uhasama ulipozuka siku mbili zilizopita, huku waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiishutumu Iran kwa kuwalenga raia.

“Iran italipa gharama kubwa sana kwa mauaji ya kukusudia ya raia, wanawake na watoto,” alisema Netanyahu wakati alipotembelea eneo la shambulio la kombora kwenye jengo la makazi katika mji wa pwani wa Bat Yam, karibu na Tel Aviv.