Baraza la usalama la Israel linakutana kujadiliana kuhusu uwezekano wa kutanua operesheni zake za kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza, hatua ambayo ikiwa itakubalika itatekelezwa licha ya upinzani mkali kutoka ndani.
Hatua hii pia inapingwa na familia za mateka wa Israel waliosalia mikononi wa wanamgambo wa Hamas.
Mkutano huu unafanyika katika siku ambayo kunaarifiwa vifo vya Wapalestina 29 kufuatia mashambulizi la anga na ardhini kote kusini mwa Gaza, hii ikiwa ni kulingana na vyanzo vya hospitali. Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis imesema imepokea miili 12 ya watu waliouawa karibu na kituo cha kupokea misaada kinachoratibiwa na Marekani na Israel. Karibu watu 50 walijeruhiwa.
Afisa mmoja wa Israel anayefahamu suala hilo alisema Baraza hilo linatarajiwa kufanya mjadala mrefu na kuidhinisha upanuzi wa mpango wa kijeshi wa kudhibiti sehemu zote au maeneo ya Gaza ambayo bado haijayadhibiti.
Afisa huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina akisubiri uamuzi rasmi, amesema chochote kitakachoidhinishwa kitatekelezwa hatua kwa hatua, kama njia ya kuongeza shinikizo kwa Hamas.
