Israel imesema mahusiano yake na Ujerumani yameathirika kutokana na uamuzi wa Berlin kuzuia kuipelekea Tel Aviv sehemu ya silaha kwa hoja kuwa zinaweza kutumika kwenye Ukanda wa Gaza.
Balozi wa Israel nchini Ujerumani, Ron Prosor, alisema uamuzi wa Berlin kusimamisha kwa sehemu fulani usafirishaji wa silaha zake kwa Tel Aviv umeyatia doa mahusiano baina ya washirika hao wa jadi, ingawa hilo halimaanishi kuwa mahusiano yamevunjika kabisa kabisa.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Welt siku ya Jumanne (Agosti 12), Prosor alisema hata kama ni sawa kuupinga mkakati wa Israel kwenye vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina, lakini si sawa kuiwacha nchi yake ikiwa haina ulinzi wowote.
“Badala ya kujadili njia za kulinyang’anya silaha kundi la wanamgambo wa siasa kali wa Kipalestina wa Hamas, sasa kuna mazungumzo ya kuinyang’anya silaha Israel. Hii ni sherehe kwa Hamas.” Alisema balozi huyo.
Wiki iliyopita, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani alitangaza kwamba nchi yake haitaipelekea tena Israel silaha ambazo zinaweza kutumika kwenye Ukanda wa Gaza.
“Uamuzi huu unatokana na mipango ya Israel kutanuwa operesheni zake za kijeshi ndani ya mamlaka ya Palestina”, alisema Merz akikusudia ukaliwaji tena kimabavu wa Jiji la Gaza.
Hata hivyo, kansela huyo wa Ujerumani alisisitiza kuwa usitishaji huo hauthiri kabisa vifaa kwa kijeshi kwa ajili ya mifumo ya ulinzi wa anga na baharini wa Israel.
