Jeshi la Israel limewataka Wapalestina kuondoka kwenye mji wa Gaza City na kuhamia katika eneo ambalo imesema ni “salama” kwao lililopo upande wa kusini.
Amri hiyo ilitolewa wakati jeshi hilo linatanua kampeni ya kijeshi kwenye mji huo ulio mkubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza.
Jeshi hilo hivi sasa linafanya mashambulizi makali ikiwemo kuyalenga majengo ya ghorofa ikiwa ni sehemu ya operesheni yake kubwa ya kutaka kuukamata mji huo.
Sehemu ya mji huo wenye wakazi wanaokaribia milioni 1, inazingatiwa kuwa uwanja wa mapambano, na imetolewa amri ya watu kuondoka kabla ya kuanza mashambulizi makali zaidi ya kijeshi.
Mashirika ya misaada ya kiutu yameonya mara kadhaa kwamba kuhamishwa idadi kubwa ya watu kutoka mji huo kutazidisha madhila na balaa ambavyo tayari Wapalestina wanashuhudia tangu kuanza kwa vita vya Gaza.
Mji wa Gaza City umeorodheshwa kuwa kwenye kitisho cha kukumbwa na baa la njaa na tayari malaki ya Wapalestina wameshalazimika kuyakimbia maakazi zaidi ya mbili tangu kuanza kwa vita.
Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee ameandika katika ukurasa wa X kuwa Al-Muwasi kuliko na kambi iliyojengwa kwa mahema kusini mwa Ukanda wa Gaza ndio salama kwa watu kwenda.
