JESHI la Israel limeanzisha mashambulizi yake ya ardhini yaliyokuwa yakisubiriwa katika Jiji la Gaza, baada ya mashambulizi makubwa ya angani usiku wa kuamkia leo katika mitaa kadhaa ya jiji hilo.
Msemaji wa jeshi hilo amesema kufuatia maagizo ya uongozi wa kisiasa, vikosi vya Israel vimetanua operesheni ya ardhini dhidi ya ngome ya Hamas katika jiji hilo.
Aliongeza kuwa operesheni hiyo inayojumuisha pia mashambulizi ya angani, yanalenga kutokomeza wapiganaji wa Hamas wanaojificha katika mahandaki mengi yaliyoko chini ya jiji hilo lenye takriban wakaazi milioni moja na ambalo ndilo kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza . Awali, Israel ilitoa tahadhari kwa wakaazi wa jiji hilo kuondoka.
Israel inakadiria kuwa kuna takriban wanamgambo 3,000 wa Hamas katika jiji hilo.
Katika tukio jingine, Israel imeshambulia mji wa bandarini Hodeida nchini Yemen. Jeshi la Israel limesema limeshambulia miundo mbinu ya kijeshi inayotumiwa na waasi wa Kihouthi katika bandari ya Hodeida.
Msemaji wa waasi Wahouthi Yahya Saree amesema mifumo yao ya ulinzi wa angani inajaribu kuzuia ndege za Israel zinazofanya mashambulizi aliyoita kuwa uchokozi dhidi ya taifa lake.
