Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewasisitiza waajiri kwenye vyombo vya habari nchini kuzingatia kikamilifu masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, hususan wanapoajiri au kuwasainisha mikataba watumishi wa kada ya habari, ili kuepuka migogoro ya kisheria inayoweza kujitokeza baadaye.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, tarehe 20-21 Januari, 2026 wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi katika mikoa ya Dodoma na Iringa, ilipotembelea vyombo kadhaa vya habari kwa lengo la kukagua kiwango cha uzingatiaji wa Sheria hiyo kwa watumishi wanaojihusisha na shughuli za kihabari, wakiwemo wahariri, waandishi wa habari, watangazaji, wapiga picha waandaaji na waandishi wa kujitegemea.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Wakili Kipangula amesema Bodi imebaini uwepo wa waandishi wenye sifa stahiki kwa mujibu wa Sheria kwenye vyombo hivyo, lakini bado hawajajisajili katika Mfumo wa TAI-HABARI ili kuomba ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari, hali inayoweza kuwaweka waajiri na waajiriwa katika hatari ya kukiuka Sheria.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa waajiri kuhakikisha kuwa watumishi wote wa kada ya habari wanakuwa wamekamilisha taratibu za usajili na kupata ithibati kabla ya kupewa majukumu au kuajiriwa ili kulinda uhalali wa ajira na kuepuka athari za kisheria.

Aidha, Wakili Kipangula amesema changamoto nyingine iliyobainika katika baadhi ya vyombo vya habari ni malipo madogo ya posho au mishahara kwa waandishi, hali inayohitaji mjadala mpana na mikakati maalum ya pamoja kati ya waajiri, wadau wa habari na Serikali ili kuhakikisha mazingira bora na ya haki ya kazi kwa waandishi wa habari.

Hata hivyo, amepongeza baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari waliobainika kuzingatia kwa umakini masharti ya Sheria, kushughulikia changamoto za waandishi wao kwa uwazi, na kufanya uwekezaji mkubwa unaolenga kujenga mazingira wezeshi, salama na rafiki ya utendaji wa kazi za kihabari.

Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, juhudi hizo ni mfano wa kuigwa na zinachangia moja kwa moja katika kulinda hadhi ya taaluma ya habari, kuongeza weledi wa waandishi na kuimarisha uaminifu wa vyombo vya habari kwa jamii.