Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, ameendelea kuonesha dhamira yake ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi kupitia kampeni yake ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao”, inayolenga kuhakikisha kila kijiji kinapata zahanati.

Leo, akiwa katika zoezi la kushukuru wananchi wa Kitongoji cha Kola, amechangia tofali 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya itakayohudumia wakazi wa eneo hilo.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu, hasa kwa wajawazito, watoto na wazee ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya karibu na makazi yao.

Dkt. Jafo amesema kampeni hiyo inalenga kukamilisha ujenzi wa zahanati katika kila kijiji ndani ya Jimbo la Kisarawe, akisisitiza kuwa huduma za afya ni haki ya msingi kwa kila mwananchi na zinapaswa kupatikana kwa urahisi bila usumbufu.

Mbunge huyo ameendelea na juhudi hizo akikusudia kuendeleza mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, ambapo aliweza kuhamasisha ujenzi wa zahanati 27 kupitia ushirikiano wa Mfuko wa Jimbo, Halmashauri, Serikali Kuu pamoja na wadau wa maendeleo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masaki, Mhe. Pili Kondo Chamgui, amempongeza Dkt. Jafo kwa juhudi zake za dhati katika kuwajali wananchi, akieleza kuwa kwa sasa vijiji vyote vya kata hiyo vina zahanati na pia kuna Kituo cha Afya cha Masaki kinachotoa huduma za upasuaji.

Amesema ujenzi wa zahanati katika Kitongoji cha Kola utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo ambalo liko mbali na kijiji mama cha Kisanga, hali iliyokuwa ikiwasababishia wakazi kusafiri zaidi ya kilometa sita kufuata huduma za afya.

Nao, Wananchi wa Kitongoji cha Kola wameeleza shukrani zao kwa mbunge huyo wakisema amesikia kilio chao cha muda mrefu cha ukosefu wa huduma za afya karibu na makazi yao, jambo lililokuwa likiwaweka katika hatari hasa wakati wa dharura za kiafya.

Kampeni ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao” inaendelea kuleta matumaini mapya kwa wananchi wa Kisarawe, huku juhudi za viongozi na ushirikiano wa jamii vikionekana kuwa chachu muhimu ya kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.