Na Mary Gwera – Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amesema kuwa, Usuluhishi haupaswi kuitwa njia mbadala ya utatuzi wa migogoro kwakuwa ni njia mojawapo inayotambulika kikatiba.
Mhe. Masaju ameeleza hayo jana tarehe 09 Aprili, 2026 wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Wiki ya Usuluhishi nchini iliyofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee jijini Dar es Salaam.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 107(A)(2)(d) ambayo inaitaka Mahakama kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro, hii ni njia halali ya utatuzi wa migogoro, kwahiyo tunachokifanya hapa kina uhalali wa kikatiba, sasa kitu kipo kwenye Katiba, kitakuwaje njia mbadala, hata usuluhishi ni njia ya kufikia haki,” amesema Jaji Mkuu.;
Mhe. Masaju amesema kuwa, Usuluhishi ni njia muhimu kwa kuwa una faida nyingi na pia unatambulika katika katika dini kuu mbili (Ukristo na Uislamu) huku akirejea Kitabu cha Mathayo Sura ya 5:9 imeandikwa kwamba, Heri Wapatanishi maana wataitwa Wana wa Mungu.
Vilevile, amerejea katika Kitabu cha Quran Tukufu (Quran: 9-10) inasema, “Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatanisheni…. Hakika waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.”
“Maneno haya matakatifu yanatufundisha kuwa usuluhishi wa migogoro kwa njia ya upatanishi ambayo ni moja ya mbinu za usuluhishi wa migogoro si takwa la kisheria pekee, bali ni msisitizo unaoelezwa pia katika vitabu vyetu vitakatifu,” ameeleza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju amewataka Wasuluhishi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, kuwajibika ipasavyo na kuvaa vazi la kiMungu wanapotekeleza jukumu hilo muhimu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amezitaja pia njia za usuluhishi wa migogoro kwa njia za asili kwa kuzingatia mila na desturi za jamii husika kama njia mbadala ni kusema kuwa, njia hizo pia ni muhimu kuziendeleza kwakuwa hata katika kiapo cha Majaji kinawataka kuzingatia na kuheshimu mila na desturi zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika hilo, Jaji Mkuu amesema kuna haja ya kufanyia marekebisho Sheria ya Serikali za Mitaa ili kuwatambua na kuwapa mamlaka ya kisheria Machifu ambapo pamoja na mambo mengine, watafanya usuluhishi kisheria kwakuwa wao pia husaidia kuhimiza uzingatiwaji wa usalama wa jamii, maadili ya jamii, amani katika jamii na umoja wa Kitaifa.
Mhe. Masaju amesema kuwa, kupitia Sheria hiyo ana imani kuwa, Machifu watafanya vizuri katika usuluhuhishi mfano wa masuala ya ardhi, ndoa na kadhalika.
Ameongeza kwamba, Mahakama ya Tanzania inaunga mkono Taasisi au wadau wote wanaotumia njia halali zinazoleta Suluhu ili mradi kutekeleza masharti ya Katiba na Sheria ili watu waishi kwa amani, utulivu na udugu.
Aidha, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, suala la kuendeleza matumizi ya njia za usuluhishi wa migogoro linaendana sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inajengwa katika msingi mkuu wa utawala bora, amani, usalama na utulivu.

“Usuluhishi ni moja ya nyezo inayolenga katika kuleta amani, usalama na utulivu. Hivyo, katika kutekeleza msingi wa Dira ya 2050 hii jukumu la wadau na Mahakama ni kuhamasisha na kuhakikisha usuluhishi unatumika ipasavyo pale migororo inapojitokeza katika jamii na shughuli za kibiashara,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ametaja Vipaumbele vinne vya Dira hiyo kuwa ni pamoja na; Utawala Bora na Haki, Serikali za Mitaa Imara na zenye ufanisi, Utumishi wa Umma Unaowajibika na Amani, Usalama na Utulivu.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ametoa rai kwa Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kuandika vitabu kwa kuwa hazina kubwa ipo kwenye vitabu, hivyo ni muhimu kufanya hivyo.
“Nirejee tena kuwashauri Majaji, Mahakimu na Watumishi wote wa Mahakama, wale mlio na uwezo wa kuandika, andikeni hazina kubwa ipo kwenye vitabu na sio kwenye hizi ‘electronic devices’ambazo hata hazina uhakika tu wa kuwepo kwa hiyo tukiandika tunasaidiana,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amekishukuru na kukipongeza Kituo cha Usuluhishi wakishirikiana pamoja na wadau kwa kufanikisha kuandaa Wiki ya Usuluhishi nchini sambamba na Watoa mada wote walioshiriki katika majadiliano.
Akitoa neno la utangulizi katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma amesema uanzishaji wa wiki ya usuluhishi ni mkakati mmoja wapo wa kuelimisha umma kuhusu uwepo wa sheria hizi na fursa zilizopo za kumaliza migogoro inayojitokeza kwa njia za usuluhishi bila ya ulazima wa kufika Mahakamani.
“Uzinduzi huu ni moja ya tukiomuhimu na la kihistoria nchini kwetu katika kukuza mfumo wa utoaji haki na kuendeleza juhudi za kitaifa katika kukuza utamaduni wa kutatua migogoro kwa njia za Usuluhishi,” amesema Mhe. Maruma.
Jaji Mfawidhi huyo amesema kuwa,Wiki ya Usuluhishi ni moja ya mkakati wa kukuza uelewa na kuhamasisha utekelezaji wa matakwa ya sheria mbalimbali zinazotoa fursa ya usuluhishi wa migogoro kabla ya kuifikisha Mahakamani.
“Wakati nchi jirani wanaweka juhudi za kutunga sheria za usuluhishi, Tanzania imekuwa mfano bora wa kuwa na sheria nyingi zaidi ya ishirini na nne zinazotoa fursa ya matumizi ya usuluhishi zikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (Sura ya 33 Marejeo 2023), Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi (Sura ya 216), Sheria ya Ndoa (Sura ya 29, Marejeo ya 2023), Sheria ya Mabaraza ya Kata (Sura ya 209), Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini (Sura ya 366), Sheria ya Ndoa (Sura 29), Sheria ya Migogoro ya Bima Sura ya 394, Toleo la Marejeo la 2023, Sheria ya Bima za Magari Sura ya 169 (2023), Sheria ya Mikataba Sura ya 345 (2019) na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Sura ya 161 (2023),” ameeleza Jaji Maruma.
Ameongeza kuwa, Matumizi ya usuluhishi hususan njia ya upatanishi ni moja ya mikakati wa Mahakama kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama kutoka mwaka 2015-2020/2021 – 2025/26 lengo likiwa ni kuharakisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri kama vile ada za mawakili na mud awa wadaawa ambaounaweza kutumika katika shughuli zingine za kiuchumi. Vile vile kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, kuongeza ufanisi, na kutoa haki inayogusa mazingira halisi ya wananchi haraka mapema ipasavyo.

“Uanzishaji wa wiki ya usuluhishi ni mkakati mmoja wapo wa kuelimisha umma kuhusu uwepo wa sheria hizi na fursa zilizopo za kumaliza migogoro inayojitokeza kwa njia za usuluhishi bila ya ulazima wa kufika Mahakamani,” amesema Mhe. Maruma.
Amesema, lengo na chimbuko la kuanzisha Wiki ya Usuluhishi nchini ni moja ya utekelezaji wa maelekezo ya Jaji Mkuu ambayo amekuwa ukiyatoa mara kwa mara katika kuhakikisha tunatekeleza jukumu la kikatiba chini ya ibara ya 107A (2) (d) la kukuza na kuendeleza matumizi ya usuluhishi.
Wiki ya Usuluhishi nchini kwa mwaka huu imebeba kaulimbiu isemayo; ‘Kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro kama mbinu inayopendelewa nchini Tanzania,’ inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili, 2026 nchi nzima na inalenga kuelimisha umma kuhusu sheria za usuluhishi kwa ujumla, kuhamasisha matumizi ya usuluhishi na kadhalika.
Wadau mbalimbali wa Kituo cha Usuluhishi wameshiriki katika hafla hiyo na baadhi yao wameshiriki kutoa uzoefu katika kazi ya Usuluhishi.







