Na WMJJWM-Dodoma
Serikali inaendelea na juhudi za kuchochea maendeleo katika jamii kupitia afua mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu masuala ya mila na desturi zinazofaa na zile zisizofaa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Neema Ndoboka wakati akifungua kikao cha wadau wanaotekeleza eneo la mila na desturi katika Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili zidi ya Wanawake na Watoto (MTAKKUWA) kilichofanyika leo (tarehe17, Septemba 2025) jijini Dodoma.

Neema amewaasa wadau wa maendeleo kuongeza juhudi zaidi na kutokukata tamaa kwani suala la jamii kukubali kuachana mila walizorithishwa vizazi baada ya vizazi si jambo jepesi.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango wenu katika kuleta mabadiliko katika jamii lakini suala mila na desturi linachukua muda hivyo mnapaswa kutokukata tamaa na inabidi muendelee kupambana zaidi kutoa elimu kwa wanajamii na madaliko yatakuja tu” amesema Neema.
Aidha, Neema ametoa wito kwa jamii kukumbatia mila na desturi zinazofaa kwani baadhi ya mila ndiyo asili ya mwafrika na zina umuhimu wake katika kulinda maadili na mienendo ya jamii.
“Tunachokipinga ni mila zinazokandamiza na kuumiza baadhi ya makundi katika jamii kwani tunaelewa kwamba kuna mila na desturi ambazo zinazofaa na zinajenga misingi ya jamii husika na maadili ya kitanzania”amesema Neema.

Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Carlos Gwamagobe amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau wa maendeleo katika kuahikisha jamii inapata elimu ya kuweza kupambanua mila na desturi zinazofaa, hivyo, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuweza kufikia malengo yake na kuhakikisha mabadiliko chanya
yanapatikana katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Naye Mratibu wa MTAKUWWA kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Alex Shayo amesema mpaka sasa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinaendelea kupungua baada ya jamii kupata elimu na kuhusiana na madhara ya mila na desturi zisizofaa.
Nao wadau wa maendeleo wanaotekeleza afua hiyo wameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake katika kutokomeza mila na desturi potofu na kuahidi kuendelea kupambana ili kuleta fikra chanya na jamii inayojitambua kwa ujumla.


