Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imemuhukumu mkazi wa Kijiji cha Ighombwe,Tarafa ya Sepuka,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida,Emanueli Musa (27) kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka binti wa darasa la tano (jina tunalo) katika shule ya msingi Ighombwe.

Mwendesha Mashtaka,wakili wa serikali Mkoa wa Singida,Nehemia Kilimuhana amedai kwamba Nov,12,mwaka 2023 akiwa katika Kijiji cha Ighombwe,Tarafa ya Sepuka,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida,Emanueli Musa alimbaka binti mwenye umri wa miaka 13 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Ighombwe,huku akijua kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Aidha katika shauri hilo la jinai lililofunguliwa katika Mahakama hiyo Aprili,11,mwaka 2023 na kusajiliwa kwa namba 8699/2025 lilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi,Bwana Allu Nzowa na aliposomewa shitaka hilo mshitakiwa alikana na ndipo upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wanne ambao walitoa ushahidi bila kuacha shaka yeyote kuwa mshitakiwa huyo ndiye aliyetenda kosa hilo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka huyo  mshitakiwa Emanueli Musa alijitetea mwenyewe na ndipo baada ya Mahakama kusikiliza pande zote mbili ilimtia hatiani kwa kosa hilo la kubaka na hivyo ili liwe fundisho kwa watu wenye tabia kama ya mshitakiwa,Mahakama hiyo ilimuhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 13.