Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa

Mahakama ya Wilaya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu kwenda jela miaka 30  na kulipa fidia ya milioni 5 atakapomaliza kifungo Evarist Justin Chamtepa (44)  mkazi wa kijiji Cha Nkomolo kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kufikia wa umri wa miaka 14.

Akitoa hukumu hiyo juzi hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya Nkasi Denis Luwungo alidai kuwa anamtia hatiani mtuhumiwa baada ya ushahidi uliotolewa na baada ya mtuhumiwa kukiri kutenda kosa hilo

‎Katika shitaka lililosomwa katika mahakama hiyo ya kesi Namba 1615 ni kuwa mtuhumiwa alimbaka mtoto wake wa kufikia baada ya kutokea mzozo wa kifamilia na mkewe kukimbilia kwa wifi yake ambako alilala Hadi asubuhi na mtuhumiwa kupata nafasi ya kutenda kosa hilo.

‎Hivyo alitenda kosa hilo chini ya kifungu 130 (1) na kifungu Cha 2 (e) na 131 (1) Cha sheria ya kanuni ya adhabu ( Penal Code) 16 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

‎Baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na mtuhumiwa kukiri kutenda kosa hilo na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu alitenda kosa hilo akiwa amelewa ndipo hakimu alimtia hatiani kwa kifungo hicho Cha miaka 30 jela na kutakiwa kulipa fidia ya Mil 5 atakapomaliza kifungo chake

‎Sambamba na hilo mahakama hiyo imemhukumu kwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko 6 Magnus Marko (22) mkazi wa Kasonso baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka binti wa miaka 15 mkazi wa Isunta wilayani Nkasi.