Watu wawili wanahofiwa kukwama baada ya jengo la orofa 16 lililokuwa likijengwa kuporomoka katika eneo la South C jijini Nairobi.
Operesheni ya uokoaji inayohusisha vitengo tofauti ikiwa ni pamoja na wanajeshi, polisi, huduma za dharura za kaunti ya Nairobi na Kenya Power inaendelea katika eneo la tukio.
Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, tukio hilo lilitokea mapema asubuhi, na kuwaacha wafanyikazi wawili wamekwama katika eneo hilo.
“Eneo hilo limezingirwa huku Kitengo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga, Kaunti ya Jiji la Nairobi, Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya wakiendelea na shughuli za utafutaji na uokoaji,” ilisoma ujumbe wa Kenya Red Cross kwenye mtandao wa X.


