Na Cresensia Kapinga, JamuhuriMedia, Songea

Mgombea Ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Jimbo la Peramiho halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Jenista Mhagama ameendelea na mikutano ya Kampeni kukiombea kura za kishindo CCM ifikapo Oktoba 29 mwaka huu,huku akimtolea sifa lukuki Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo. 

Akizungumza  Jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Mdunduwalo kata ya Maposeni na kijiji cha Litowa kilichopo kata ya Parangu, Mhagama alisema kuwa kuna kila sababu za kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo. 

Alisema kuwa Rais Samia ameonesha uongozi wa kipekee  na usio na kifani katika kuhakikisha ahadi za chama zinatimia kwani katika uongozi wake ameweza kukamilisha na kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi ikiwemo miradi ya afya, miundombinu ya barabara, elimu, maji,umeme pamoja na kilimo.

” Dkt.  Samia siyo tu Rais wa kwanza mwanamke, bali pia ni kiongozi mwenye maono makubwa,anayesikiliza na kuchukuwa hatua, katika kipindi hiki cha uongozi wake ameonesha kuwa Tanzania inawezekana, sasa ni wakati wetu kuhakikisha kazi hii inaendelea kwa kumpa nguvu kupitia Sanduku la kura ” alisema Mhagama. 

Mhagama pia alitaja baadhi ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika Jimbo la Peramiho, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya Afya, barabara za vijijini, upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote vya Jimbo hilo, upatikanaji wa maji safi na salama, upatikanaji wa mbolea pamoja na mbegu za Ruzuku kwa wakulima.

Kwa upande wao wananchi waliohudhuria mikutano hiyo ya kampeni wameahidi kuwapigia kura za kishindo wagombea wa CCM katika nafasi zote,Urais, ubunge na madiwani na kwamba wamejionea miradi mbalimbali ya maendeleo ikitekelezwa kwenye kata zao kwa vitendo.

Awali mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Thomas Masolwa akiwanadi wagombea wa nafasi ya udiwani na mbunge katika Jimbo la Peramiho alisema kuwa licha ya wagombea kupita bila kupingwa lakini kuna hadui mmoja ambaye ni “Hapana” hivyo wananchi wasifanye makosa wanapiga kura za hapana.

Alisema wananchi wao ni mashahidi wa mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt.Samia katika sekta ya afya na elimu ambapo amehakikisha kwamba watoto wa kitanzania wanapata elimu bora kupitia ujenzi wa shule mpya na maboresho katika miundombinu ya shule za zamani halikadhalika sekta ya afya upatikanaji wa huduma bora na ujenzi wa hospitali za kisasa,vituo vya afya pamoja na zahanati.