Na Cresensia Kapinga, JamuhuriMedia, Songea

Mgombea ubunge wa Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jenista Mhagama amewaahaidi wananchi wa kata ya Ndongosi, kuwa Serikali itajenga barabara ya zege kwenye maeneo korofi yenye miinuko na utelezi ili kuhakikisha barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 126 kutoka Songea mjini ambayo ndio tegemeo kwa wananchi wa kata hiyo inapitika kipindi chote cha masika.

Ahaadi hiyo ameitoa jana wakati akihutubia mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza wakati wa ziara yake ya kampeni ya kusaka kura za kishindo kwenye uchaguzi mkuu ujao Oktoba 29, mwaka huu ambapo amewaomba wananchi wa kata hiyo kumchaguwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, mbunge pamoja na diwani wa chama hicho.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk.Samia Suluhu Hassan imesikia kilio chao na tayari Serikali kupitia wakala wa Barabara vijijini (TARURA) imetenga fedha kwa ajili ya kujenga sehemu korofi kwa zege hasa kwenye maeneo ya miinuko na kwenye maeneo yenye utelezi ili barabara hiyo iweze kupitika kipindi chote cha masika na kiangazi.

Alisema kuwa tayari barabara hiyo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na tayari imeshaingizwa kwenye Ilani ya chama lengo ni kuimarisha miundombinu ya usafiri na kuondoa adha ambayo wananchi wamekuwa wakiipata kwa muda mrefu kutokana na ubovu wa Barabara hiyo.

Kwa upande wao wananchi wa kata ya Ndongosi inayounda vijiji vitatu vya Nambendo, Namatuhi na Ndongosi wamefurahishwa na ahadi hiyo ambapo wamesema kuwa barabara hiyo imekuwa kikwazo kwa shughuli za kijamii na kiuchumi hasa wakati wa masika.

Nae mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Thomas Masolwa alitumia nafasi hiyo kumnadi mgombea ubunge na udiwani huku akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020/2025 kazi zilizokwisha fanyika kwenye kata hiyo ikiwemo, sekta ya afya, elimu, maji, umeme na miundombinu ya barabara kwenye baadhi ya maeneo yamekwisha fanyika.

Aidha ameelezea Ilani ya CCM ya mwaka 2025/30 ambapo alisema kuwa miradi yote ambayo wananchi wa kata hiyo wanahitaji imeandikwa, ikiwemo barabara,ujenzi wa kituo cha afya cha kisasa katika kijiji cha Nambendo, ujenzi wa chumba cha kujifungulia akina mama katika zahanati za vijiji vya Ndongosi na Namatuhi, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za msingi na sekondari.

Pia umeme vitongoji vyote vilivyobaki, usambazaji wa maji,upatikanaji wa pembejeo za kilimo za ruzuku na Ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka, hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kuwapigia kura wagombea wa Chama cha Mapinduzi na si vinginevyo.